Pichani wajumbe mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Rukwa, Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo, Nkasi
na Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia Mkutano wa kwanza wa majaribio ya huduma
ya Video Conference leo katika ukumbi wa "Video Conference" uliopo katika Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Anayeonekana kwenye Luninga akiwasilisha mada ni Naibu
Katibu Mkuu Utumishi Ndugu Hab Mkwizu ambao ndio walioandaa mkutano huo
uliojadili mada mbalimbali.
******
Mkoa wa Rukwa
ni miongoni mwa Mikoa iliyowezeshwa kuwa na Miundombinu ya huduma ya "Video
Conference" ambao unaratibiwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Huduma hii muhimu itasaidia sana katika kurahisisha mawasiliano Serikalini na
hivyo kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji
huduma kwa wananchi.
Katika majaribio ya awali
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetoa mada mbalimbali kupitia
mfumo huo kwa Makatibu Tawala pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa kwa Mikoa ya Rukwa, Mara, Lindi, Ruvuma na
Shinyanga.
Miongoni mwa mada hizo
zilizowasilishwa zikifuatiwa na majadiliano ni Utekelezaji wa Mfumo wa "OPRAS"
katika Utumishi wa Umma, Mwenendo wa utekelezaji wa masuala Anuai za jamii
katika Utumishi wa Umma, Usimamizi na uzingatiaji wa Maadili ya Utumishi wa Umma
na Mafanikio na Changamoto za utekelezaji wa Mfumo wa Taarifa za kiutumishi na
Mishahara Serikalini.
Zoezi hili la
majaribio limefanikiwa japo kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo kukatika
kwa mawasiliano yanayounganisha picha na sauti sababu kubwa ikiwa ni Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kukosa huduma za Mkongo wa Taifa unaoratibiwa na Wizara ya
Mawasiliano, Sayanisi na Teknolojia.
Changamoto nyingine ni
baadhi ya picha kuwa na muonekano hafifu, ambayo kwa mujibu wa Mchambuzi wa
Mifumo ya Komputa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Ndugu Emmanuel Mwandiga
inasababishwa pia na kasi ya huduma za mtandao kuwa chini pamoja na masafa ya
mawasiliano kuwa hafifu.
Changamoto hizo zikifanyiwa
kazi na Wizara husika ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ni wazi kuwa mfumo
huo utakua njia sahihi zaidi na kisasa inayokwenda na wakati katika kurahisisha
na kuboresha mawasiliano Serikali.
Wajumbe wakifuatilia mada kwa makini kupitia Luninga
kubwa iliyopo mbele yao (Video Conferencing) Mambo yalikuwa yanakwenda "LIVE"
ikiunganishwa Mikoa ya Rukwa, Lindi, Mara, Ruvuma, Shinyanga na Dar es Salaam
ilipo Wizara ya UTUMISHI.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (wapili
kushoto) nae alikuwepo kushuhudia Mkutano huo wa majaribio ambapo alipewa dakika
kumi kuchangia juu ya mfumo huo ambapo alisema Serikali itaokoa fedha nyingi
kuliko ilivyokuwa hapo awali ambapo wajumbe kutoka Mikoa mbalimbali walikuwa
wakilazimika kusafiri kwa magari ya ofisi kuhudhuria vikao nje ya mikoa na
maeneo yao ya kazi kwa gharama kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (kushoto)
na Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima wakifuatilia moja ya mada
iliyokuwa ikiwasilishwa kupitia mfumo huo mpya wa "Video
Conferencing".
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga
Ndugu William Shimwela akichangia moja ya mada katika mkutano huo. Kulia ni
Muhasibu Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ndugu Sosthenes
Mutarubukwa.
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Ndugu Samson Mashalla akichangia moja ya mada katika
mkutano huo.
(Na Hamza Temba - Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa Rukwa)
0 comments:
Post a Comment