SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, October 10, 2013

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA:UTENDAJI KAZI WA BOYA LA MAFUTA LA SINGLE POINT MOORING (SPM) KIGAMBONI, DAR ES SALAAM


Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mafuta kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Capt. Abdul Mwingamno akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu ufanisi wa mradi wa SPM Ikiwa ni pamoja na kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 150,000,Wakati wa Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.

Picha na Frank Mvungi
--
MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA
 UTENDAJI KAZI WA BOYA LA MAFUTA LA SINGLE POINT MOORING (SPM) KIGAMBONI, DAR ES SALAAM
---

UTANGULIZI
Mradi wa ujenzi wa boya jipya lijukanalo kama Single Point Mooring (SPM) pamoja na miundombinu ya kusafirisha mafuta ulianza mwaka 2010 na kukamilika mwezi Novemba 2012. 

GHARAMA YA MRADI
Mradi huu uligharimu kiasi cha dola za Marekani millioni 70.5 sawa na Shilingi bilioni 113 za Tanzania.

UWEZO WA BOYA
SPM ina uwezo wa kuhudumia meli zenye ujazo wa tani 150,000 za mafutana tangu boya hilo limezinduliwaNovemba 2012 mpaka Agosti 2013 limehudumia mafuta safi (white products) jumla ya tani 1,529,411 na tani 513,787 za mafuta ghafi wakati mafuta yaliyohudumiwa na Kitengo cha Mafuta cha Kurasini (KOJ) katika kipindi cha Novemba 2012 mpaka Agosti 2013 ni tani 1,503,298.

Kukamilika kwa mradi huu, kunaiwezesha Bandari kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 150,000 (DWT) hivyo kuongeza tija katika kuhudumia meli za mafuta. Tofauti na boya la awali SPM sasa inaweza kupokea na kusukuma mafuta safi (white products) na ghafi (crude oil) kwa wakati mmoja. 

Mradi wa SPM unaiwezesha nchi kupakua mafuta kwa kutumia meli kubwa zenye uzito wa 150,000 (DWT) ukilinganisha na zile zinazoleta mafuta katika gati la mafuta la Kurasini (KOJ) zenye uzito wa 45,000 (DWT).

MAFANIKIO/UFANISI
Tangu SPM mpya ianze kufanya kazi mnamo tarehe 15 Novemba 2012, yamepatikana mafanikio makubwa hasa katika kupunguza msongamano wa meli za mafuta uliokuwepo miaka iliyopita. Msongamano huo ulikuwa ni kero kubwa kwa wadau wa bandari na waagizaji mafuta nchini.

Msongamano huo uliibebesha Serikali mzigo mkubwa wa kulipa gharama ijulikanayo kama ‘demurrages’ ambayo wenye meli hutozabaada ya meli kusubiri muda mrefu kufunga kwenye gati la KOJ.

Gharama hiyo ilifikia hadi Dola za Kimarekani 50 kwa kila tani moja. Lakini kutokana na maboresho yaliyofanyika yameweza kupunguza gharama za demurrages hadi Dola za Kimarekani 1.2 kwa kila tani. Hayo ni mafanikio makubwa ambayo yamekuja baada ya kupunguza siku za meli kusubiri zamu toka wastani wa siku 45 hadi siku 1.

Kwa kuwa kituo cha Mafuta cha Kurasini (Kurasini Oil Jetty – KOJ) kinaendelea kutoa huduma sambamba na SPM mpya, uwezo wa kuhudumia meli umeongezeka kwa kuwezesha kuhudumia meli mbili hadi tatu kwa wakati mmoja. Hiyo ikiwa na maana kuwa kila kituo kinaweza kupakuwa aina tofauti ya mafuta na hivyo kuongezea ufanisi na tija.

Mafanikio zaidi yanategemewa muda si mrefu kwa kupunguza siku za kupakuwa mafuta SPM mara makampuni ya mafuta yatakapomaliza uboreshaji wa mabomba yao hadi kufikia kipenyo cha nchi 12, ikiwemo makampuni ya mafuta ya Kigamboni kuweka bomba maalum la kupokelea mafuta moja kwa moja kutoka SPM badala ya kupitia KOJ ambako kutokana na umbali unasababisha kasi ya ujazo kwa saa kupungua.

UTENDAJI KAZI WA BOYA
Meli zinafungwa kwenye boya ambalo liko kwenye kina cha maji cha mita 25.5 (CD) ambapo bomba la 24” linaleta mafuta ya Dieseli mpaka Kigamboni ambapo linaunganika na bomba la 18” kuleta mafuta mpaka KOJ na kusambazwa kwa wenye matanki ya kuhifadhia mafuta.

Mafuta ghafi (crude oil) yanatolewa kwenye meli na kupitisha kwenye bomba la 28” urefu wa bomba ni kilometa 3.7 majini na kilometa 4.3 nchi kavu mpaka Kigamboni na kilometa 2 kutoka Kigamboni mpaka KOJ.

Mafuta ya Petroli, mafuta ya taa (Kerosine), Mafuta ya ndege (Jet A1) na baadhi ya mafuta ya Dieseli bado yanapitishwa KOJ.

Mipango ya TPA, ni kukarabati boya la zamani ili mafuta ya Petroli nayo yapitie SPM.

Mabomba ya kuleta mafuta ya Petroli (dock lines) yameongezwa na manifold mpya za Dieseli na Petroli kujengwa SPM. Mabomba ya kuleta mafuta ya chakula nayo yameongezwa KOJ.

Ili kuongeza kasi ya kupakua mafuta kutoka SPM, TPA inajenga manifold mpya huko Kigamboni kwa ajili ya OMCs waliopo Kigamboni.

MABORESHO ZAIDI
Awamu ya pili ya mradi wa SPM itatekelezwa kati ya mwaka 2014 na mwaka 2016 na itahusisha ujenzi wa matenki ya kupokea mafuta kwa muda (custody transfer tanks) na kugharimu dola za Marekani milioni 60 sawa na shilingi billion 96 za Tanzania.

MCHANGO WA SPM KATIKA UPATIKANAJI WA MAFUTA NCHINI

Boya la zamani la SPM lilikuwa linahudumia mafuta ghafi (crude oil) tu kwa ajili ya Zambia na hapa nchini. Lakini mradi wa SPM umewezesha Boya jipya la SPM kuhudumia mafuta ghafi na mafuta safi (white products).

Endapo mradi wa boya jipya usingefanyika tungekuwa tumehudumia
jumla yatani 2,017,085 tu za mafuta yaliyosafishwa na
yasiyosafishwa sawa na asilimia56.9, lakini kutokana na boya jipya la
SPM kuhudumia tani 1,529,411 za mafuta sawa na asilimia 43.1
tumeweza kuhudumia jumla ya tani 3,546,446 katika kipindi cha
kuanzia Novemba 2012 mpaka Agosti 2013.

MWISHO
Tunawasihi wananchi wote tushirikiane katika kulilinda na kulitunza
boya hili ambalo limeigharimu Serikali na Mamlaka fedha nyingi ili liwezkuleta manufaa kwa uchumi wetu na wananchi kwa ujumla. 

Imetolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
S.L.P. 9184
DAR ES SALAAM

0 comments:

Post a Comment