SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, October 20, 2013

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA CHAMA CHA WANANCHI(CUF):CUF HAIHUSIKI KATIKA HOJA YA VYAMA KUTOWASILISHA HESABU ZAKE OFISI YA MKAGUZI MKUU WA SERIKALI.

 Julius Mtatiro
 
Chama Cha Wananchi CUF kinapenda kuwajulisha watanzania kwa ujumla kuwa, kimetekeleza sheria mbalimbali ambazo zinataka vyama vya siasa vipeleke hesabu zake ili zikaguliwe na vyombo maalum vya serikali.

Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa kifungu cha 14, vyama vilivyo na usajili wa kudumu vinatakiwa kuwasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa hesabu za kila mwaka zilizokaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali(CAG). Sheria hii ina maana kuwa kwa CAG vyama vinapita kama PROCESS na kwamba kwa MSAJILI ndipo hasa vyama vinapaswa kupeleka ripoti ya hesabu zilizokaguliwa na CAG.

Hiyo ina maana kuwa vyama sasa vinawasilisha hesabu zisizokaguliwa kwa CAG na CAG ambaye ni ofisi ya serikali ana jukumu la kufanya ukaguzi mpana zaidi mpaka ajiridhishe na hiki ndicho CUF imekuwa ikitekeleza.

Hesabu za mwisho ambazo CUF imeziwasilisha kwa MKAGUZI MKUU WA SERIKALI ni zinazoishia tarehe 31/12/2011 ambapo ziliwasilishwa tarehe 11/09/2012 kupitia barua yenye kumbukumbu namba CUF/AK/DSM/KM/OO3/1A/2012/39 iliyosainiwa na MKURUGENZI WA FEDHA WA CUF ndugu. Salim Mandari iliyokuwa na kichwa cha habari “KUWASILISHA HESABU ZISIZOKAGULIWA KWAKO KWA AJILI YA UKAGUZI HESABU ZINAZOISHIA 31/12/2011”.

Hatua hii ilitokana na kutekeleza sheria pamoja na maelekezo ya barua ya msajili wa vyama vya siasa iliyokuwa na kumbukumbu namba CDA.112/123/01A/37 ambayo ilimtaka Katibu Mkuu wa chama chetu awasilishe hesabu zisizokaguliwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kama hatua ya MSAJILI kukimbusha chama.

Tumesikitishwa na kauli tulizozisikia kupitia katika vyombo vya habari kuwa chama chetu ni miongoni mwa vyama kadhaa ambavyo havijawasilisha hesabu kwa mkaguzi mkuu wa serikali kwa kipindi cha miaka minne sasa. Tunaomba watanzania wazipuuze taarifa hizo kutuhusu kwa sababu hazina ukweli wowote.

Chama Cha Wananchi CUF pia kinapenda kuujulisha umma kuwa hesabu zake ambazo hazijawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ni zile zinazoishia tarehe 31/12/2012 ambazo wakaguzi wa ndani na wa nje wamemaliza kuzikagua mwezi Julai mwaka 2013 na zitathibitishwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa cha mwezi Oktoba 2013 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokaa mwezi Novemba 2013 na kisha zitawasilisha kwa CAG kabla ya mwezi Desemba 2013. Hii ina maana kuwa hesabu ambazo hazijamfikia msajili ni za mwaka mmoja uliopita na siyo miaka minne kama ambavyo kamati ya PAC imetangaza.

Chama chetu kimesikitishwa na kufadhaishwa na hatua ya kamati kuvihukumu vyama vyote vya siasa wakati jambo hili ni la chama kimoja kimoja. Na mbaya zaidi ni pale ambapo mwenyekiti wa kamati ya PAC mhe. Zitto Kabwe amekuwa akishinda kwenye mitandao ya kijamii “akishupalia” kuvichukulia hatua vyama – kikiwemo chama chetu huku hana taarifa za kina za namna tulivyotekeleza wajibu wetu.

Ikiwa kamati ya bunge inashinda kwenye mitandao ya kijamii ikihukumu na kutoa taarifa za uongo kwa umma bila hata kuwasiliana na vyama vya siasa ni jambo la kufedhehesha mno. Kamati makini ya bunge ni ile ambayo inapokea taarifa kutoka pande zote muhimu, inakutana na wadau wote na kisha inajua tatizo liko wapi na kuujulisha umma nani amesababisha uzembe.

Kwa sababu kamati hii imeligeuza jambo hili kuwa mtaji wa kisiasa na kukitangaza chama chetu kuwa hakikutambua wajibu wake jambo ambalo siyo sahihi, Chama chetu kinatafakari hatua za kuchukua ikiwemo kumuandikia Spika ili azifundishe kamati zake namna bora ya kufanya kazi zake kama kamati za umma.

Chama chetu pia hadi leo hakijapokea barua yoyote ya kuitwa na kamati ya bunge ya hesabu za serikali siku ya tarehe 25 Oktoba. Kwa hiyo, CUF haitahudhuria katika kikao hicho kwa habari za kuitiwa kupitia kwenye FACEBOOK, TWITTER, WHATS UP n.k.

Kama kamati inatuhitaji twende kuifafanulia taarifa za upande wa pili baada ya kumaliza kazi yake ya kutuchafua, na ituandikie barua rasmi ya kutuita tarehe 25, tukipata barua tutakwenda. Ikiwa hatuitwi tarehe hiyo kwa barua rasmi hatutakwenda na kamati ya PAC haitakuwa na "LOCUS STAND" ya kutuhoji mahali popote pale.

Tunapenda watanzania waelewe kuwa chama chetu kimekuwa pekee ambacho kimepata hati safi za ukaguzi wa fedha kila mara tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi na hatukuwahi kupata doa wala kashfa katika masuala ya fedha.

Mungu Ibariki Tanzania!



“HAKI SAWA KWA WOTE”
Julius Mtatiro,
National Deputy Secretary General,
The Civic United Front(CUF),
Tanzania Mainland,
P.O Box 10979,
Dar Es Salaam.
Phone; +255717536759,

Email; juliusmtatiro@yahoo.com
Twitter; https://twitter.com/Julius_Mtatiro
Fb; https://www.facebook.com/julius.mtatiro

0 comments:

Post a Comment