Rais
Jakaya Kikwete akimsalimia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa
Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja wakati akiwasili
kuzindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa Mkongo wilayani Rufiji
hivi karibuni. Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo,
Profesa Lucian Msambichaka na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula
na Ushirika, Bw. Yamungu Kayandabila (kwanza kushoto).
Na Mwandishi wetu, Pwani
Rais
Jakaya Kikwete amesema kambi ya vijana ya kilimo na Maarifa Mkongo
iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani iwe moja ya mifano hai ya kuondoa
umaskini na kuwakomboa wananchi kivipato.
Rais
Kikwete ametoa changamoto hiyo alipokuwa akifungua rasmi kambi hyo
iliyobuniwa na Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) hivi karibuni
wilayani Rufiji.
“Umasikini
wa watu wetu utaondoka kupitia jitihada kama hizi zenye dhamira ya
kuwakomboa kivipato,” alisema na kuongeza kuwa vijana hao wakitumia
ujuzi waliopata kwa vitendo watabadilika kimaisha na watakuwa mfano kwa
jamii yote. Alisema kambi hiyo ni nzuri kwa vijana na haina budi kutoa
mafunzo ya kilimo ambayo yatawawezesha kwenda kujiajiri na siyo kusubiri
ajira ili wakaeneze ujuzi huo katika maeneo wanayotoka.
Kambi
ya vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo ni moja ya njia za utekelezaji
wa azma ya serikali ya kuleta mapinduzi ya kijani Kupitia mpango wa
Kilimo Kwanza.
Kambi
hiyo imeanza na vijana 50, kati ya hao wavulana wakiwa 36 na wasichana
14. Rais alisisitiza kwamba vijana hao watakapomaliza mafunzo yao
wawezeshwe ili watakaporudi katika vijiji vyao wakatumie ujuzi
walioupata kwa vitendo kupata fedha.
“Hawa
wakitoka hapa wasiachwe tu, mkiwaacha muda mfupi mtawakuta wanacheza
pool…hivyo ufanyike utaratibu maalumu wa kuwawezesha kwa usimamizi
maalumu ili mashamba yao yakawe kivutio kwa watu wengine kupenda
kilimo,” alisema.
Akitoa
mfano alisema mazao nyanya, tikitimaji na matango ya shamba darasa ya
kambi hiyo yana soko kubwa, hivyo watakapomaliza mafunzo hayo wakatumie
ujuzi huo kulima mazao hayo ili kufanikiwa.
Pia
aliitaka RUBADA na Wizara ya Kilimo na Ushirika kuhakikisha wanatafuta
aina bora ya mbegu inayozaa mazao mengi ili vijana hao wakafurahie kazi
hiyo na kuwavutia wenzao na jamii nzima.
Akiongea
wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa RUBADA, Bw. Aloyce
Masanja alisema kambo hiyo pia ni utekelezaji wa mpango wa kukuza kilimo
katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ambao unalenga kuleta
mapinduzi ya haraka ya kilimo kikanda unaojumuisha jitihada na nguvu za
pamoja za wadau mbalimbali.
RUBADA
inatekeleza mpango huu kwa mtindo wa “Hub and Spoke” ambapo mwekezaji
mkubwa wa ndani au wa nje anakuwa “Hub” na wakulima wadogo wanakuwa
“Spoke” wote kwa pamoja wakisukuma gurudumu la maendeleo.
Akifafanua
zaidi alisema mtindo huu unahusu kuanzisha kambi za vijana kwa kila
eneo lenye mwekezaji mkubwa katika bonde zima la mto Rufiji linaloanzia
mkoa wa Pwani, Morogoro, Iringa, Mbeya, sehemu ya Dodoma, Singida,
Ruvuma na Lindi.
Bw.
Masanja alisema kufuatana na mkakati sa SAGCOT uliobainisha kongani sita
za Rufiji, Kilombero, Ihemi, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga; RUBADA,
imeandaa mpango kabambe wa utekelezaji ambao utashirikisha vijana katika
kila kongani. “Kwa mwaka huu wa fedha, tunategemea kuwa na vituo vitano
vya vijana katika kilimo na maarifa na kila kituo kitakuwa na vijana
wasiopungua 300 ambao watapata mafunzo katika kipindi cha mwaka mmoja,”
alisema.
Vituo
hivyo vya vijana vitakuwa na majukumu ya kutoa mafunzo kuhusiana na
utekelezaji wa kilimo bora chenye tija; kuongeza thamani mazao; matumizi
ya vifaa vya kisasa; utekelezaji wa kilimo bora bila uharibifu wa
mazingira; kuandaa andiko la mradi ili kuweza kupata mikopo katika
taasisi za fedha na uundaji wa vikundi vya ushirika.
Kwa
mujibu wa Bw. Masanja, mafunzo katika kambi hizo yatajikita katika
maeneo makuu matatu yakihusisha uzalishaji wa mazo ya kilimo kwa wingi
na yenye thamani kubwa hasa mazao ya bustani, mboga mboga na matunda;
ufugaji wa kisasa wa ng’ombe na kuku na ufugaji wa samaki pamoja na
ujasiriamali.
“RUBADA
inatarajia kuzalisha vijana 600 kutoka kituo cha Mkongo hadi 2015 ambao
watakuwa na utaalamu na ujuzi wa kilimo chenye tija na ufugaji wa
kisasa,” alisema Mkurugenzi huyo.
Kilimo
ni moja ya sekta zinazolengwa katika mikakati mbalimbali ya serikali
katika mapinduzi ya kiuchumi na kufikia malengo ya Milenia na Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya 2025. Kulingana na sense ya watu ya 2012, asilimia
60 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana.
NA MICHUZI MATUKIO
NA MICHUZI MATUKIO
0 comments:
Post a Comment