SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, May 23, 2013

SHULE ZA KATA ZAJIENDESHA KWA FEDHA ZA WALIMU WAKUU

 
 Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Nduweni, Venance Mramba  
Mkuu wa Sekondari ya Tanya, Victus Kiwango
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya 

****
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Rombo kimesema shule nyingi za Sekondari za Kata wilaya hiyo na maeneo mengine nchini zinajiendesha kwa kutegemea fedha za mifukoni kwa walimu wakuu wanaoziongoza shule hizo. 



Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu wa CWT Wilaya ya Rombo, Erasmo Mwingira alipokuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi. Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni kwa kutembelea shule kadhaa za sekondari wilayani hapa umebaini kuwepo na mazingira magumu ya uendeshaji wa shule hizo kutokana na ugao wa fedha za uendeshaji shule hizo kutokuwa wa uhakika huku hata kiasi kinachozifikia hakitoshelezi gharama za uendeshaji.



 Akifafanua Mwingira alisema fedha zinazotolewa kuziendesha shule hizo ‘capitation’ licha ya kuwa hazitoshi huwa hazifiki kabisa shuleni hali ambayo huwafanya walimu wakuu kubuni mbinu mbalimbali za uendeshaji wa shule zao ikiwemo kuweka utitiri wa michango kwa wazazi ili kuhakikisha mambo yanakwenda shuleni. 



“Sasa hivi shule za msingi na sekondari (za serikali) zinaendeshwa na mifuko ya walimu wakuu…capitation haifiki kabisa shuleni, fedha inayowafikia ni kidogo sana na haiwezi kuendesha zile shule, walimu wanatumia mbinu zao kuziendesha shule ndio maana unaona michango inakuwa mingi shuleni,” alisema Mwingira.Alisema licha ya serikali kusema ada ya sekondari ni shilingi 20,000 kwa sasa michango katika shule hizo ni mingi kiasi cha kufikia 120,000 jambo ambalo limewafanya baadhi ya wazazi kuelemewa na mzigo wa michango na wengine kushindwa kabisa kuimudu.



Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi katika shule za Sekondari za Tanya, Nduweni, Urauri, Holili na Ngaleku na nyinginezo zote za wilayani Rombo umebaini uwepo wa utitiri wa michango jambo ambalo limelalamikiwa na baadhi ya wazazi na wadau wa elimu wilayani hapa. Mfano shule ya Sekondari Tanya jumla ya michango yake imefikia sh. 115,000; mgawanyiko wake ukiwa kama ifuatavyo:- Ada sh 20,000, Madawati sh 15,000, Chakula sh 60,000, Tahadhari sh 5,000, Ulinzi 5,000, Taaluma sh 5,000 na Kitambulisho sh 5,000. 



Aidha uchunguzi zaidi umebaini shule nyingi za sekondari za kata hazina walimu wa masomo ya sayansi jambo ambalo huwalazimisha walimu wakuu kutafuta walimu wa kukodi hasa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kuja kuwafundisha wanafunzi masomo ya sanyansi kama Hisabati, Fizikia, Kemia, Baiolojia na mengineyo huku wakitumia mbinu anuai kukusanya michango kuwalipa walimu hao wa kukodi. 



“Nashauri Serikali iongeze fungu la uendeshaji wa fedha shuleni maana fedha za michango zinazotolewa na wazazi hazitoshi kuendesha shule…huwa tunakodi walimu (wanafunzi waliomaliza kidato cha sita) kuja kutufundishia masomo ya sayansi kwa muda unakuta gharama zinakuwa kubwa za uendeshaji shule,” alisema Mkuu wa Sekondari ya Tanya, Victus Kiwango. 



“Sisi tumelazimika kuajiri kwa muda wanafunzi sita waliomaliza kidato cha sita kufundisha masomo ya sayansi kwa fedha za shule…tunajibanabana kwa michango pamoja na wazazi na kuhakikisha tunapata chochote kuwalipa walimu hawa wa muda bila hivyo mambo hayaendi,” alisema Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Nduweni, Venance Mramba akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Kwa upande wake Mwingira alisema vijana wa kidato cha sita ambao hutumiwa na shule nyingi kuokoa jahazi ya masomo ya sayansi wamekuwa wakiwakaririsha wanafunzi kujibu mitihani na sio kuwafundisha jambo ambalo alisema ni hatari kwa elimu ya Tanzania. 



“Kujua kusoma na kuandika si kigezo cha kumfundisha mtu…vijana hawa wa kidato cha sita hawana mbinu za ufundishaji wanachokifanya ni kuwakaririsha wanafunzi. Pamoja na hayo aliishauri serikali kutojitoa katika jukumu la kuendesha shule za kata na kuwaachia wazazi kwani shule hizo ziko katika hali mbaya na zinahitaji kuongezewa fedha za uendeshaji. 



Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya alikiri kuwepo na tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi katika shule nyingi za wilaya yake, hivyo walimu kulazimika kuajiri kwa muda vijana wa kidato cha sita kusaidia wanafunzi huku jitihada zikiendelea kufanya kukabiliana na tatizo hilo. 



 “Walimu wa sayansi ni tatizo Rombo hawatoshi…mwaka huu tumejitahidi na kuajiri takribani walimu 134 wakiwemo wachache wa masomo ya sayansi lakini tatizo bado lipo,” alisema Mboya kikilitolea ufafanuzi suala hilo ofisini kwake wilayani Rombo hivi karibuni. CHANZO: www.thehabari.com

0 comments:

Post a Comment