SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, February 7, 2012

‘WE LOVE YOU HARISSON’ NI MANENO YA WANANCHI WALIOSHUHUDIA .........!!

Dk. Harrison Mwakyembe kabla ya kuugua.
Dk. Harrison Mwakyembe baada ya kuugua.
Elvan Stambuli na Makongoro Oging'
“WE love you Harrison,” yalikuwa ni maneno ya baadhi ya wananchi walioshuhudia kwa mara ya kwanza, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe akihutubia katika Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Wananchi hao walifikia hatua ya kusema hivyo wakimaanisha kuwa bado wanampenda licha ya hali waliyomuona nayo Dk. Mwakyembe ambaye alionekana kuzeeka, ngozi kuchubuka na kuwa mweupe, huku nywele zake zikiwa zimenyofoka na kumfanya afiche kichwa kwa kuvaa kofia aina ya pam.
Hata hivyo, kilichompata katika mikono yake ni siri yake kwani muda wote alikuwa amevaa glovu nyeusi.
Wakizungumza na gazeti hili katika Viwanja vya Tanganyika Packers, baadhi ya wananchi walionesha wazi kumsikitikia kiongozi huyo ambaye alionesha ujasiri mkubwa alipokuwa akishughulikia sakata la kampuni ya kufua umeme ya Richmond na kupiga vita ufisadi nchini.
Agnes John, alisema amesikitika kumuona kiongozi huyo akiwa katika hali aliyonayo sasa na kuongeza: “Inasikitisha, kwa vyovyote huyu mbunge amelishwa sumu kama wenzake wanavyodai.”

Wananchi wengi walionesha simanzi yao kutokana na hali ya kiafya ya Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela. Mwandishi wetu wa Mbeya anaripoti kuwa picha zilizoonekana katika vyombo vya habari zikimuonesha kiongozi huyo akiwa katika viwanja hivyo, ziliwatoa machozi wapiga kura wake wa Jimbo la Kyela.
Licha ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kusema hadharani kuwa Mwakyembe amelishwa sumu, serikali kwa upande wake imekuwa ikimtaka kiongozi huyo kupeleka vithibitisho vya madai yake ili ifanye uchunguzi.
Ugonjwa wa Dk. Mwakyembe umefanywa kuwa siri licha ya kupelekwa India alikopatiwa matibabu ya afya yake na kulazwa katika hospitali maarufu nchini humo ya Indraprastha Apollo iliyopo mjini Chinai.
Akiwa huko, Balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi alipohojiwa na wanahabari ugonjwa unaomsumbua naibu waziri huyo, aligoma kutaja kwa maelezo kwamba hajapata ripoti kamili ya daktari wake.
Kabla ya kuondoka nchini, mke wa Dk. Mwakyembe, Linah Mwakyembe alinukuliwa akisema, “…Tatizo la mwili kuvimba, lilianza miezi mitatu iliyopita. Linakuja na kupotea. Lakini sasa naona kama hali inazidi kuwa mbaya.”
Dk. Mwakyembe aliondoka nchini akiwa amevimba mwili mzima.
Mwanasiasa huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa wakati alipoteuliwa kuongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond, hajawahi kulalamika kuumwa isipokuwa amewahi kuripoti hofu ya usalama wake.

KUTAKA KUHONGWA MILIONI 50/=
Tangu kusomwa bungeni ripoti ya Richmond, Februari 2008, Dk. Mwakyembe amekuwa akidai kufuatwafuatwa ikiwemo mbinu za kutaka kumuua kwa njia mbalimbali.
Wakati wa maandalizi ya ripoti ya Richmond kuwasilishwa mbele ya mkutano wa bunge, taarifa zinamnukuu Dk. Mwakyembe akisema walikuwepo watu waliotaka kumhonga shilingi milioni 50 ili afiche ukweli.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, akiwamo Lucas Selelii ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Nzega (CCM), walidai kwamba kilitengwa kitita cha shilingi milioni 10 kwa kila mjumbe ili kuwalainisha.

BARUA YA KURASA SABA
Hata hivyo, Februari 9, 2011, Dk. Mwakyembe aliandika barua yenye kurasa saba kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema akisema kuna genge la watu limepanga njama za kumuua na katika waraka huo maalum alioupa kichwa cha habari, ‘Taarifa ya njama za kuondoa maisha yangu na ombi kwa jeshi la polisi kulinda haki yangu ya kikatiba ya kuishi,’ Dk. Mwakyembe aliwataja watu wengine saba katika orodha ya wanaotakiwa kuuawa (majina tunayahifadhi.)
Kuhusu malalamiko yake kwa IGP Mwema, Dk. Mwakyembe alisema: “Pamoja na kwamba taarifa hii ni mpya yenye matukio ya takribani mwezi mmoja tu (wakati huo), naamini kwa dhati kuwa msingi wake, kwa maana ya wahusika na maudhui, hautofautiani na ule wa matukio mengine ya awali ambayo baadhi yake yalisharipotiwa polisi na vyombo vingine vya usalama kwa lengo la kuchunguzwa.”
Pamoja na kuthibitisha kupata barua ya malalamiko ya Dk. Mwakyembe, IGP Mwema alisema walikuwa wanafanyia kazi malalamiko hayo. Hakutoa taarifa zaidi bali alielekeza aulizwe Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa Polisi (DCI), Kamishna Robert Manumba kwa maelezo zaidi.
Hofu ya Dk. Mwakyembe kutishiwa maisha, ilikuja chini ya miaka miwili tangu apate ajali ya gari iliyomtikisa taya lake ingawa hali yake iliimarika.
Ajali hiyo ilitokea Ihemi, Iringa akiwa kwenye gari lake aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 362ACH akitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam.

NAPE NNAUYE
Naye Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye alipozungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema kuna kila dalili ya Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu na kutafutwa na maadui zake.
“Nasikitika kuona serikali haichukui hatua na kusikiliza malalamiko yake. Siku anakwenda India Mwakyembe alinipigia simu, nikampeleka uwanja wa ndege, mwili wake ulibadilika na ulikuwa ukitoa unga,” alisema.
Nape alihoji kama ugonjwa wake ni wa kawaida kwa nini hapa nchini usionekane na madaktari? Aliishauri serikali kuweka wazi jambo hilo ili kuondoa utata uliopo sasa kwa kuwa Mwakyembe ni mtu anayesimamia haki na huu unyama amefanyiwa na mafisadi walioifilisi nchi.
Alisema kwa upande wake yupo tayari kuwa naye bega kwa bega kupambana na ufisadi.
CHANZO: BOFYA HAPA

0 comments:

Post a Comment