Mbunge mmoja wa Uganda ameurejesha muswada wenye utata wa wapenzi wa jinsia moja, lakini kipengele cha hukumu ya kifo kimeondolewa, kwa kosa la vitendo kadhaa.
Mwandishi wa BBC amesema wabunge walicheka, kupiga makofi na kushangilia wakisema "Muswada wetu, muswada wetu," wakati mbunge huyo David Bahati alipourudisha tena bungeni siku ya Jumanne.
Muswada wa wapenzi wa jinsia moja uliwekwa kando mwaka 2011 kufuatia malalamiko kutoka jumuiya ya kimataifa.
Kukaa kimya
Bado muswada huo unabeba adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kukutwa na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Kufanya mapenzi ya jinsia moja ni kosa la kisheria nchini Uganda - katika jamii ambayo ina msimamo mkali - ambapo wengi hulaani mapenzi ya jinsia moja.
Yeyote anayemfahamu mtu anayefanya mapenzi ya jinsia moja na kukaa kimya bila kusema kwa mamlaka, pia huenda akashtakiwa.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala, Joshua Mmali, amesema Bw Bahati, ambaye ndio aliyeanzisha hoja ya muswada huo amethibitisha kuwa muswada huo umebadilishwa kwa kiasi kikubwa.
Misaada
Wale wote watakaokutwa na kosa la "mapenzi hatari ya jinsia moja" - yaani kama mmoja wa washiriki ni mtoto mdogo, au ana maambukizi ya HIV, mlemavu, au "anayefanya hivyo mara nyingi" - hatakabiliwa na adhabu ya kifo, kama ilivyopendekezwa awali.
Kamati ya bunge imependekeza kufanywa kwa marekebisho hayo, baada ya sheria ya awali kushutumiwa na viongozi wa nchi za Magharibi, akiwemo Rais wa Marekani Barack Obama aliyesema sheria hiyo kuwa ni "mbaya", na kutishia kufuta misaada kwa Uganda.
Bw Bahati ana matumaini kuwa muswada wake binafsi hatimaye utajadiliwa katika kikao cha sasa cha bunge, ambacho kimeanza siku ya Jumanne.
Makundi
Mbunge huyo ni kiongozi wa vikao vya chama kinachotawala katika bunge, na hivyo mapendekezo ya sheria kamwe yasingeweza kuwasilishwa bila ya serikali kuunga mkono, anasema mwandishi wetu.
Muswada huo uliwasilishwa kwanza mwaka 2009, lakini haukuwahi kujadiliwa katika bunge.
Katika miaka ya hivi karibuni, makundi kadhaa ya wapenzi wa jinsia moja yameanzishwa nchini Uganda.
Mwezi Januari mwaka 2011, mwanaharakati wa wapenzi wa jinsia moja, David Kato, aliuawa katika kile baadhi ya watu wanasema ni uhalifu wa chuki, ingawa polisi walisema lilikuwa tukio la ujambazi.
Katika mazishi ya mwanaharakati huo, mchungaji alilaani wapenzi wa jinsia moja.
Chanzo: BOFYA
0 comments:
Post a Comment