SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, January 31, 2012

VITUKO VYA MASTAA MAJUU: MCHEZA SINEMA AJIUA ILI KUOMBOLEZA NA KUPINGA KUUAWA KWA MBWA WAKE!!!

Mcheza sinema huyo kwenye picha anaitwa Nick Santino (47). Jana (28/1/2012) aliamua kubugia makumi ya vidonge na kuacha ujumbe akilalamika kuhusu kuuawa kwa mbwa wake aitwaye Rocco. Rocco ilibidi auawe baada ya wamiliki wa jumba alimokuwa akipanga kule jijini New York kupinga wapangaji wake kuwa na majibwa makubwa (pitbulls) kama Rocco. Baadhi ya wapangaji wenzake pia walilalamika kwamba Rocco alikuwa akibweka sana.
Kwa wenzetu hawa mbwa ni sehemu ya familia na hivyo hutunzwa na kugharamiwa kama vile memba wengine wa familia. 
Mbwa wengine huwa na bima ya afya, hupelekwa kwa daktari kufanyiwa uchunguzi wa afya zao kila mwaka na kupatiwa chanjo mara kwa mara na wakati mwingine huweza hata kuachiwa urithi. Na mbwa anapofariki, familia nzima huwa na huzuni kwa kuondokewa na memba wa familia.
Jirani yangu hapa alifiwa na mbwa wake aliyekuwa amekaa naye kwa miaka 13. Watoto wake walihuzunika sana kiasi kwamba ilibidi wapatiwe ushauri nasaha. Nasi ilibidi kuwatumia kadi za kuwapa pole na kuwatia moyo!
Kwa sisi Waafrika kisa kama hiki cha mtu kujiua eti kwa sababu ya mbwa wake kufariki linaweza kuonekana kuwa jambo la kuchekesha. Katika makabila mengi mbwa walifugwa hasa kwa lengo la kusaidia katika uwindaji na ulinzi wa nyumba au mifugo. Nakumbuka siku nilipowaambia wanafunzi wangu Wamarekani kwamba kijijini nitokako mbwa hapaswi kulala ndani ya nyumba bali nje ili kuhakikisha kuwa mifugo na familia iko salama. 
Wanafunzi hao walishangaa na wengine waliona kuwa ilikuwa ni ukatili kuwalaza mbwa nje ya nyumba.
Inabidi tujibidishe kujifunza na kuziheshimu tofauti hizi za kitamaduni hasa katika wakati huu ambapo dunia inazidi kufungamana zaidi. Ni dalili ya ujinga kucheka na kudharau tamaduni zingine hata kama zinaonekana kuwa ngeni, za "kishenzi" na kushangaza namna gani. Baadhi ya tofauti za kitamaduni kati ya Waafrika na wazungu zimeeelezwa vizuri katika kitabu mashuhuri cha Profesa Mbele kiitwacho
Africans and Americans: Embracing Cultural Differences

0 comments:

Post a Comment