-Wanaharakati nao wawasha moto Dar es Salaam
-Muswada ukisomwa kwa mara ya pili kuandamana
-Wasema hakuna yeyote atakayeweza kuyazima
Mkutano wa Tano wa Bunge unaendelea leo huku mjadala mkali ukitarajiwa kuibuka hasa wakati wa kuchangia Muswada wa Katiba.
Muswada wa Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, unatarajiwa kuwasilishwa leo kwa mara ya pili na tatu, na kujadiliwa kwa siku tatu mfululizo.
Licha ya wadau mbalimbali kutaka usomwe kwa mara ya kwanza kwa maelezo kuwa ni mpya kutokana na kuondolewa bungeni Aprili, mwaka huu na kufanyiwa marekebisho, serikali imesema kuwa muswada huo utasomwa kwa mara ya pili na ya tatu.
Uamuzi huo ulishatolewa na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisisitiza msimamo huo juzi wakati akifungua semina ya wabunge kuhusu muswada huo.
Bado wabunge wamegawanyika kuhusu muswada huo hususani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Upinzani.
Habari zinasema kuwa wajumbe wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala, walikuwa wamegawanyika wakati wa kuupitia muswada huo kuhusu madaraka aliyopewa Rais ya kuunda Tume ya katiba na kuitisha Bunge la Katiba.
Katika kuhakikisha kuwa muswada huo haupati upinzani, wabunge wa CCM walikutana Ijumaa iliyopita kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja wa kuuunga mkono.
Hata hivyo, wabunbe wa upinzani walionyesha wasiwasi wao kuhusu muswada huo wakati wa semina ya Jumamosi katika mada zilizowasilishwa na Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi, na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Profesa Romwald Haule.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema maelezo yaliyotolewa na Profesa Kabudi, kwamba hakuna sababu za kuhofia madaraka ya rais kwa sababu kuna kuaminiana na yale yaliyotolewa na Kamati ya Sheria na Katiba na Profesa Issa Shivji kwamba muswada huo unampa rais madaraka makubwa yanampa wasiwasi.
Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala iliwaalika Profesa Shivji; Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na kuipa uzoefu kuhusu katiba kwa wiki moja jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Bunge.
Kafulila alisema ni lazima wabunge watazame ukubwa wa madaraka ya rais kwa sababu haiwezekani kutenganisha siasa na utawala na kutahadharisha kuwa: “Kufanya hivyo ni kuwa na dola na sio umma.”
Akijibu hoja ya Kafulila, Profesa Kabudi alisema kwa kawaida wasomi hutofautiana katika hoja.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, naye alieleza wasiwasi wake ikiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ya sasa ndiyo itakayoratibu kura ya maoni ya kuamua katiba, akisema kuwa hatua hiyo baadaye inaweza kuleta mifarakano kwa kuwa Nec ya sasa haikubaliki.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alihoji sababu za watoa mada kutoeleza kuhusu muswada wenyewe.
Lissu pia alihoji madaraka ya rais kwa kusema: “Tume ya Katiba haina shida, tatizo hapa itakuwaje inatunga rasimu ya katiba na kumpelekea rais kabla ya idara ya kisekta na wizara na wananchi kujadili?”
Mbunge pekee wa CCM ambaye licha ya kukubaliana na muswada huo, alipendekeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ashauriane na Rais wa Zanzibar wakati wa kuunda tume ya Katiba bila kuwashirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Kuna kila dalili kwamba mjadala wa muswada huo utakuwa mkali na wabunge watauchangia kwa itikadi za vyama vyao.
WANASHERIA NAO WAPINGA
Chama cha Wanasheria Cha Tanganyika (TLS), kimeishauri Serikali kusitisha mpango wa kusoma Muswada huo kwa mara ya pili na ya tatu ili kuhifadhi Utawala wa Sheria, amani na usalama wa Taifa.
Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jana jijini Dar ea Salaam, Rais wa chama hicho, Francis Stolla, alisema iwapo utapitishwa bungeni, “tunamshauri Rais asiridhie sheria hiyo.”
Alisema mchakato mzima wa utungwaji wa katiba unapaswa kupata uhalali muafaka kwa kushirikisha wananchi.
Stolla alisema Katiba inapaswa kutungwa kwa matakwa ya wananchi kwani jina la Muswada halitilii maanani shauku ya wananchi kupata katiba mpya.
“Bila kurekebisha kwanza Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 kutunga katiba mpya kwa matakwa ya wananchi itakuwa si halali,” alisema Stolla.
Alifafanua kuwa Muswada huo unampa mamlaka makubwa Rais wa Jamhuri na yule wa Zanzibar na kwamba ni kinyume na dhana ya utawala bora na utenganisho wa mamlaka ya umma.
Aliongeza kuwa, vipengele visivyo bayana katika Muswada huo vinaacha mianya kwa serikali kufanya maamuzi bila vigezo maalum au kwa utashi wa kigeugeu.
Aidha TSL iliishauri serikali kuufanyia marekebisho kikamilifu kwa kuainisha mapendekezo mbalimbali ya wadau pamoja na maelezo mahususi yaliyoandaliwa na chama hicho.
Mbali ya Katiba, upitishwaji wa Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2011 ambao unafuta Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2004 unatarajia kuibua mjadala mkali.
Muswada huo uliwasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, serikali ikipendekeza iruhusiwe kufanya manunuzi ya dharura na pia kununua vifaa vilivyotumika kama ndege, meli, mabehewa na injini zake kwa kujenga hoja kwamba gharama yake ni kubwa, ni vigumu kupatikana kwa urahisi vikiwa vipya na upatikanaji wake vikiwa vipya huchukua muda mrefu.
Wabunge wengi waliukosoa vikali hasa kipengele cha kununua vifaa hivyo vikiwa ‘mtumba’ wakisema kuwa manunuzi hayo yataweza kusababisha majanga na kwamba uamuzi huo utawaruhusu watendaji wasio na uadilifu kujinufaisha kwa kununua vifaa vibovu.
Muswada huo ulipangiwa kupitishwa Ijumaa jioni, lakini kutokana na msimamo wa wabunge, serikali iliuahirisha hadi leo ambapo mawaziri watajibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge.
Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alizungumza kwa jazba wakati akichangia na kuwaponda wabunge waliopinga ununuzi wa ndege, meli, mabehewa na injini zake akisema kuwa wanatumiwa.
Wiki hii pia Bunge litapokea taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini itakayowasilisha Alhamisi kuhusu uchunguzi wa sekta ndogo ya gesi asilia, suala ambalo pia huenda likazua mjadala kuhusiana na tatizo la nishati nchini na kasi ndogo ya serikali katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa kukabiliana nalo licha ya kutengewa kiasi kikubwa cha fedha.
Suala linalosubiriwa na Watanzania wengi ni ripoti ya uchunguzi ya Kamati Teule kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, aliyesimamishwa kwa tuhuma za kuchagisha fedha kutoka taasisi zilizoko chini ya wizara yake kuhakikisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/12 inapitishwa.
WANANCHI WATISHIA KUANDAMANA
Jijini Dar es Salaam, wananchi waliohudhuria mdahalo wa Katiba uliorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, wamepinga Muswada kuwasilishwa kwa mara ya pili na ya tatu, na kuonya kwamba iwapo serikali itaendelea na msimamo wake, wataandamana nchi nzima kupinga.
Mdahalo huo ambao ulianza saa 9:00 alasiri, uliwakutanisha wananchi wa kada mbalimbali wakiwemo wanaharakati na vijana.
Wananchi waliochangia mdahalo huo walizungumza kwa hisia wakitaka serikali iuwasilishe kwa mara ya kwanza ili kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni huku Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deos Kibamba, akieleza kwamba kama serikali itapuuza maoni hayo ya wananchi, jukwaa hilo litaitisha maandamano makubwa nchi nzima.
"Endapo serikali itatupuuza, tutaandaa maandamano ya nchi nzima ambayo hakuna chombo kitakachoweza kuyazima, hakuna mwanasiasa, polisi wala mtu yeyote atakayeweza kutuzuia...najua viongozi wetu ni waoga sana, wanaogopa maandamano madogo madogo ya vyama vya siasa, lakini napenda kuwaambia kwamba wasithubutu kuzuia ya Katiba." alisema Kibamba.
Katika mdahalo huo, Mwenyekiti wa Tadea, Lifa Chipaka, alinusurika kupigwa na washiriki wenzake, baada ya kuisifia Katiba inayotumika sasa na kuwataka wananchi kutotumia jazba wakati wa mchakato jambo lililoibua zomea zomea.
Hata hivyo, Kibamba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mdahalo, aliwataka washiriki wamsikilize lakini ilishindikana huku wengine wakiimba 'CCM, CCM' hali iliyomfanya anyang'anywe kipaza sauti na kutakiwa akae chini.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment