Tarehe
21 Julai, mwaka huu, 2011,Katibu Mkuu Kiongozi Bwana Phillemon
Luhanjo, akitumia madaraka yake ya Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi wa
Umma, alitangaza hatua ya kumpa likizo ya malipo Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Bwana David Kitundu Jairo, ili kupisha
uchunguzi aliokuwa ameuagiza ufanyike dhidi yake.
Bwana
Luhanjo alichukua hatua ya kumsimamisha Bw. Jairo kufuatia tuhuma
zilizokuwa zimeelekezwa dhidi yake na baadhi ya wabunge wakati wa
mjadala kuhusu Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa
mwaka 2011/12 katika kikao cha Bunge kilichofanyika tarehe 18 Julai,
2011. Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa
Wizara kuomba michango ya fedha kutoka kwenye Taasisi zilizoko chini
ya usimamizi wake ili kusaidia Bajeti ya Wizara hiyo kupita kwa
urahisi.
Kufuatia hatua hiyo ya kumsimamisha kazi Bw. Jairo, Katibu Mkuu
Kiongozi alimwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Bwana Ludovick Utouh kufanya ukaguzi maalum na uchunguzi wa
awali juu ya tuhuma hizo. Tarehe 9 Agosti, mwaka huu, 2011, Bw.
Utouh aliwasilisha Ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, na tarehe
23, Agosti, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi akiambatana na Bw. Utouh
alitangaza mbele ya waandishi wa habari matokeo ya ukaguzi huo maalum
na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma dhidi ya Bw. Jairo.
Katika Ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, Bw. Utouh
alihitimisha: “Ukaguzi maalum haukuthibitisha kuwepo kwa usahihi wa
tuhuma zilizotolewa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
Bw. David Kitundu Jairo.” Kufuatia Ripoti hiyo ya Bw. Utouh,
Katibu Mkuu Kiongozi naye aliwaambia waandishi wa habari: “Matokeo ya
uchunguzi huo ni kwamba tuhuma zilizotolewa Bungeni tarehe 18 Julai,
2011, hazikuweza kuthibitika. "Kutokana na matokeo haya ya
uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu,
Nishati na Madini, Bwana David Kitundu Jairo, sitaweza kuendelea na
hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma (notice) na Hati ya
Mashitaka kwa sababu Bwana David Kitundu Jairo, hajapatikana na kosa
la kinidhamu (disciplinary offence) kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi
Maalum.
”
Alihitimisha: “Kufuatia matokeo ya taarifa hii ya awali na kwa
mamlaka niliyonayo kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya Utumishi Umma ya
Mwaka 2002 na kanuni zake za Mwaka 2003, NINAAMURU BWANA DAVID
KITUNDU JAIRO AREJEE KAZINI KUANZIA SIKU YA JUMATANO, TAREHE 24
AGOSTI, 2011.” KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU, inapenda kutoa
ufafanuzi kuwa baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya CAG na uamuzi
wa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu suala hilo asubuhi ya tarehe 25
Agosti, 2011,
Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
aliamua kuwa Ndugu Jairo asirudi kazini mpaka kwanza yeye Rais
atapoamua namna gani ya kurudi kazini, lini na wapi.Katibu Mkuu
Kiongozi alifikisha uamuzi huo wa Rais kwa Ndugu David Jairo ambaye
mapema asubuhi ya siku hiyo alikuwa ameripoti kazini. Ndugu Jairo
alitii uamuzi huo wa Rais.
Tunapenda
kusisitiza kuwa Mheshimiwa Rais hajawa kigeugeu kwa sababu alifanya
uamuzi mmoja tu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu
Kiongozi. Na uamuzi huo aliufanya kabla ya Bunge kulizungumzia suala
hilo na hivyo uamuzi huo wa Rais haukutokana na shinikizo la Bunge.
Pamoja na kumweleza Katibu Mkuu Kiongozi, Rais pia alimfahamisha
Waziri Mkuu kuhusu uamuzi wake huo asubuhi hiyo ya tarehe 25, 2011.
Aidha,
tunapenda kufafanua zaidi kwamba Katibu Mkuu Kiongozi ametimiza
wajibu wake ipasavyo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Katibu Mkuu kwa
mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Rais, kwa upande wake,ametumia madaraka yake kama Mamlaka
ya Ajira ya Katibu Mkuu. Hakuna suala la kujichanganya wala ukigeugeu
ndani ya Serikali kuhusu suala hili.
Mwisho.
Imetolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, Dar es Salaam.
26 Agosti, 2011
0 comments:
Post a Comment