Sudan 'yahitaji mpango mpya wa mafuta'
Mfanyakazi akiwa karibu na tangi la mafuta
Kulingana na ripoti mpya, Sudan inahitaji kuwa wazi zaidi juu ya mapato yake ya mafuta ili kuendeleza usalama eneo hilo.
Shirika la Global Witness limesema mashaka juu ya mapato yalivyokuwa yakigawanywa yameongeza kiwango cha kutokuaminiana baina ya kaskazini na kusini.
Ripoti hiyo imetolewa kabla ya kura za maoni kufanyika siku ya Jumapili juu ya uhuru wa kusini.
Mafuta mengi kutoka Sudan yanatoka kwenye visima kutoka Kusini lakini miundo mbinu imebaki kaskazini.
Katika ripoti yake, Global Witness imeeleza pande zote mbili zinahitaji kukubaliana kwa uwazi zaidi ambayo itakuwa mbadala wa iliyopo kwa sasa, inayotarajiwa kumaliza muda wake mwisho wa mwezi huu.
Ripoti inasema, " Kumekuwa na kutokuaminiana hasa iwapo mfumo wa mgawanyiko wa mapato wa sasa umefanyika kwa haki."
" Shaka juu ya mgawanyiko wa mapato ndio moja ya sababu zilizofanya upande wa kusini kujitoa kwenye makubaliano ya kugawana madaraka mwaka 2007. Ushahidi unapendekeza kuwa wasiwasi huo haujathibitishwa."
Ripoti hiyo pia inasema serikali ya Sudan na kampuni kuu ya mafuta eneo hilo- China National Petroleum Corporation- hawajaeleza sababu za hitilafu katika takwimu zilizochapishwa juu ya uzalishaji.
"Ni muhimu taarifa hizi zielezwe. Makubaliano mapya ya mafuta baina ya kaskazini na kusini ni muhimu ili kuzuia kurejea kwa vita."
Kura hiyo ya maoni itakayochukua wiki nzima inayoanza siku ya Jumapili ni sehemu ya makubaliano ya mwaka 2005 iliyomaliza vita vilivyodumu kwa miongo miwili.
Zaidi ya aslimia 95 ya wapiga kura waliojiandikisha wako Sudan ya Kusini huku waliobaki ni wa kusini wanaoishi kaskazini au moja ya nchi nane za kigeni.
0 comments:
Post a Comment