SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, January 9, 2011

Jk atoa kauli mauaji ya Arusha

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali itahakikisha matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika medani ya kisiasa jijini Arusha Jumatano wiki hii, hayatokei tena.
Alitoa kauli hiyo alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini, katika hafla fupi ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2011, iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.
Rais Kikwete alisema mwaka uliopita (2010), ulikuwa wa uchaguzi, ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi.
Alisema anashukuru uchaguzi huo ulifanyika salama na kudhihirisha kwamba, demokrasia imekua nchini. Hata hivyo, alisema kuna matukio katika medani ya kisiasa yaliyolikumba jiji la Arusha hivi karibuni. “Tunatarajia matukio hayo yatakuwa ni ya mwisho kutokea,” alisema Rais Kikwete bila kutoa ufafanuzi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, alisema kuwa serikali itachukua hatua ya kuzikutanisha pande zinazohusika katika mgogoro huo kwa lengo la kuzisuluhisha.
Alisema hadi sasa maeneo mengi nchini yanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na ukame kutokana na kukosa mvua licha ya kipindi hiki kuwa ni cha mvua.
Hata hivyo, alisema ana matumaini kwamba, katika majira mengine ya mvua itapatikana katika maeneo hayo, huku akimuomba Mungu iwe hivyo.
Alisema mwaka huu Watanzania watasherehekea kutimiza miaka 50 ya uhuru, ambapo watatumia fursa hiyo kuitazama upya Katiba ya nchi.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini Ivory Coast, alimtaka Laurent Gbagbo kuachia madaraka ili kuheshimu matakwa ya wengi, ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) na wananchi wa nchi hiyo.
Naye Mkuu wa Mabalozi nchini, Juma-Alfani Mpango, akitoa salam za shukrani katika hafla hiyo, alimpongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa tena na Watanzania kuendelea na wadhifa huo.
Alisema ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, umeonyesha jinsi gani Watanzania bado wana imani naye pamoja na chama chake (CCM).
Pia alimpongeza Rais Kikwete, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kwa jitihada zao kubwa zilizowezesha kubadilisha hali ya kisiasa Zanzibar.
Alisema jitihada hizo zimefanikisha amani, utulivu na mshikamano kutamalaki hivi sasa miongoni mwa Wazanzibari visiwani humo.
Alimsifu Rais Kikwete kuwa ni kiongozi msikivu na kutolea mfano wa namna alivyopokea kilio cha wananchi cha kutaka mabadiliko ya Katiba ya nchi, ambaye ameahidi kushughulikia.

0 comments:

Post a Comment