Ukata wazuia Eto’o, Song kutua Bongo
Samuel Eto’o.
Na Wilbert Molandi
BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limeeleza kuwa kikosi cha Cameroon ambacho kina baadhi ya nyota kama Samuel Eto’o na Alexander Song, kimeshindwa kushiriki Kombe la Chalenji kutokana na ukata katika baraza hilo.
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, Cameroon ilikubali kushiriki michuano hiyo inayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu, ila ukata umekuwa kikwazo.
“Hadi sasa (juzi) tuna shilingi milioni 600 ambazo tumedhaminiwa na kampuni ya SBL, lengo ni kufikisha bilioni moja hivyo bado tunahitaji shilingi milioni 400.
Alexander Song.
“Kama tungeiongeza Cameroon, gharama za mahitaji mengine zingeongezeka, hivyo tumeonelea kuwaacha hadi mwakani maandalizi yakiwa mazuri.
“Tulikuwa tunatamani sana Cameroon iwepo ili kunogesha michuano hiyo. Hata hivyo kwa timu zilizothibitisha kushiriki zitafanya michuano kuwa na ushindani mkubwa,” alisema Musonye.
Timu waalikwa zinazotokea nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni Ivory Coast, Malawi na Zambia.
Hata hivyo, inaonekana huenda ingekuwa vigumu kwa Cameroon kuja na nyota hao hata kama ingeshiriki kutokana na kukabiliwa na majukumu kwenye klabu zao za Inter Milan ya Italia na Arsenal ya England.
Makundi yako kama ifuatavyo: A ni Somalia, Zambia, Burundi na wenyeji Tanzania Bara. B ni Rwanda, Ivory Coast, Sudan na Zanzibar na mwisho ni C lenye timu za Uganda, Kenya, Malawi na Ethiopia.
0 comments:
Post a Comment