Uchaguzi wa rais nchini Ivory Coast waingia katika duru ya pili
Uchaguzi wa rais nchini Ivory Coast waingia katika duru ya pili, baada ya kumalizika zoezi la kuhesabiwa kuwa na hakuna hata mgombea mmoja aliyeweza kufanikiwa kufikisha asilimia hamsini za kura zake. Taarifa zinasema kuwa, duru ya pili itawashirikisha wagombea wawili ambao ni Laurent Gbagbo Rais wa sasa wa Ivory Coast na Alassane Outtara Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo. Matokeo ya awali yameonyesha kuwa, Gbagbo amejipatia asilimia 38 akifuatiwa kwa karibu na Outtara aliyejipatia asilimia 32 huku Rais wa zamani wa nchi hiyo Henri Konan Bedie akijipatia asilimia 25. Hata hivyo wachambuzi wa kisiasa wanaeleza kuwa, katika duru ya pili, kura za Henry Bedie huenda zikaelekea kwa Outtara ambaye anatoka katika eneo la kaskazini lenye idadi kubwa wafuasi wa dini ya Kiislamu. Wakati huohuo, mamia ya wananchi wa Ivory Coast wafuasi wa Henri Bedie wamemiminika kwenye barabara za mji wa Abidjan wakilalamikia udanganyifu mkubwa uliofanywa kwenye zoezi la uchaguzi wa rais. Waandamanaji hao ambao wanamuunga mkono Henri Konan Bedie, wamelalamikia udanganyifu na uchakachuaji mkubwa uliofanyika kwenye uchaguzi huo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, suala la kupokonywa silaha makundi ya waasi na kuainishwa utambulisho wa wapiga kura kwenye daftari la kudumu la kupigia kura, ni miongoni mwa sababu kuu zilizopelekea kucheleweshwa kufanyika uchaguzi huo kwa muda wa miaka mitano iliyopita.
0 comments:
Post a Comment