IKRAM Athuman mwenye umri wa miezi minane, anaweza kuelezewa kuwa ni
mtoto mwenye bahati, kwani imefahamika kuwa ni miongoni mwa majeruhi
saba walionusurika kifo katika ajali ya mtumbwi uliopinduka na kuzama
juzi mjini Mtwara.
Mtumbwi huo unaofanya safari kati ya eneo la Shangani na Msangamkuu
mjini Mtwara linalotenganishwa na bahari ya Hindi kwa kilometa
zisizozidi tatu, unahofiwa kuwa umesababisha vifo vya watu 21 kati ya
28 waliokuwa wanasafiri nao.
Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Stephen Buyuya alisema jana mjini
hapa kuwa, mtoto huyo na mama yake, Fatuma Hamisi waliozama majini na
baadaye kuokolewa, ni miongoni mwa watu saba walionusurika na sasa
wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Ligula.
“Kati ya majeruhi saba, mmoja ni mtoto wa kiume mwenye umri wa
miezi minane…..kiujumla wote afya zao zinaendelea vizuri na wanaweza
kuruhusiwa kadri hali zao zinavyozidi kuimarika …hakuna mwili wowote
uliopatikana hadi sasa licha ya wazamiaji kuendelea na kazi ya
kuitafuata,” alisema Buyuya.
Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Idd Hamad, Rukia Mohammed,
Fatuma Ismail, Zainabu Ismail na Rukia Salum, wote wakazi wa
Msangamkuu.
Aidha Kamanda Buyuya alisema nahodha aliyemtaja kwa jina la Cletus
na msaidizi wake anayefahamika kama `Chaijaba’ inadaiwa waliruka baada
ya mtumbwi kuanza kupoteza mwelekeo. Mpaka sasa hawajulikani walipo.
“Inasemekana kuwa hawa wapo hai, sisi kama jeshi la Polisi
tunazifanyia kazi ….inadaiwa pia mtumbwi huo ulikuwa umetoboka na
ulizibwa kwa viroba ambavyo vinadaiwa vilizibuka na kuanza kuingiza
maji,” alisema Buyuya.
Kamanda huyo alibainisha kuwa kwa mujibu wa wataalamu miili ya watu
hao itaanza kuelea baharini leo, hivyo ametoa wito kwa wakazi wa mikoa
ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam kutoa taarifa polisi pindi
watakapoiona miili hiyo.
Sunday, May 2, 2010
AJALI YA MTUMBWI MTWARA: Mtoto wa miezi 8 anusurika kifo
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Sunday, May 02, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment