Kwa zaidi ya saa mbili, kijiji cha Mgusu wilayani Geita, Mwanza,
kinachokaliwa na wachimbaji wadogo na kuendesha shughuli zao za
uchimbaji wa dhahabu, jana kiligeuka 'uwanja wa vita’ baada ya kuibuka
mapambano baina ya wachimbaji na polisi.
Polisi hao wapo katika eneo hili wakilinda machimbo hayo
yaliyofungwa mapema mwaka jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, baada ya
kuporomoka na kuua wachimbaji wadogo zaidi ya kumi, huku wengine zaidi
ya 20 wakiripotiwa kunusurika.
Lakini chanzo cha vurugu za jana, kinadaiwa ni kuchoshwa kwa
wachimbaji hao kusubiri kufunguliwa kwa machimbo, kama ilivyokuwa
imeahidiwa na Waziri Mkuu kwamba yangefungwa kwa siku 90 tu.
Hata hivyo, baada ya kuona mwaka mmoja unavuka huku serikali ikiwa
kimya, wachimbaji hao alfajiri ya jana walijiamulia kuvamia machimbo
hayo wakiwa katika kundi la zaidi ya watu 200, wakiwamo wanaume,
wanawake na watoto.
Inadaiwa kwamba, kitu cha kwanza walichokifanya ni kuwashambulia
polisi watano waliokuwa katika lindo, wakiwarushia mawe kuwataka
waliache eneo hilo ili warudi katika uchimbaji wa madini.
Polisi nao waliamua kujibu mapigo kwa kutumia risasi za moto na
mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya wachimbaji hao waliokuwa
wanarusha mawe yaliyoonekana kuwazidi nguvu polisi hao.
Inaelezwa kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kuomba nguvu
ya ziada kutoka Kituo Kikuu cha Polisi mjini Geita na baada ya muda,
kundi la askari zaidi ya 15 waliingia eneo la tukio lililokuwa
limeshamiri mapambano.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wachimbaji wakitumia mbinu ya
kuwatanguliza mbele watoto wadogo wenye umri wa kati ya miaka 6 na 10,
kwa lengo la kusaka `huruma’ ya polisi.
Hata hivyo, polisi `hawakudanganyika’, kwani waliendelea
kuwadhibiti wavamizi hao ambao baadaye walianza kutawanyika, kila mmoja
akielekea upande wake kwa lengo la kujisalimisha.
Baadhi inadaiwa wamejeruhiwa, na mmoja ametolewa utumbo baada ya kudaiwa kupigwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi.
Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Geita aliyekuwa katika eneo la tukio
kuongoza operesheni hiyo, ACP Hassan Kimea alisema vijana wake
walilazimika kutumia nguvu kwa kuwa kitendo cha wachimbaji hao kuamua
kuwashambulia kwa mawe askari wanaolinda eneo hilo, hakitavumiliwa.
“Hatuwezi kuwakamata hawa watu wote zaidi ya 200…..lakini tuna
taarifa za uhakika tena kwa majina kuhusu watu walioratibu mipango yote
hii hadi kuifikisha katika hali hii, ni lazima tuwakamate na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria…,” alisema ACP Kimea.
Kwa upande wake Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Paul Kihimbila
alisema kuwa, katika tukio hilo askari wake kadhaa wamejeruhiwa
kutokana na kupigwa kwa mawe na wachimbaji hao, na kuongeza kwamba kwa
sasa ulinzi umeimarishwa zaidi katika eneo la tukio.
“Kwa kweli vurugu zilikuwa kubwa sana…ingawa hadi sasa hatuna
taarifa za mwananchi yeyote kupigwa risasi, lakini tuna taarifa kwamba
kuna baadhi wamejeruhiwa vibaya katika purukushani wakati wakikimbia na
wengine nasikia wamevunjika miguu, na wengine kuumizwa… Isipokuwa kuna
askari wangu mmoja ambaye nimemuona amejeruhiwa baada ya kupigwa na
jiwe kichwani, ingawa nasikia kuna wengine zaidi nao wamepigwa mawe,
lakini sijawaona…
“Kwa sasa ndiyo tunaendelea kukusanya taarifa kutoka kila upande,
lakini kuna watu naambiwa wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya
wilaya, kwa hiyo sina taarifa rasmi na nzuri kwa sasa…” alisema
Kihimbila.
Hata hivyo, kwa upande wao baadhi ya wachimbaji waliopata nafasi ya
kuzungumza na gazeti hili, walisema ugumu wa maisha umewafanya
kushindwa kuvumilia, ndiyo maana wakalazimika kutumia mabavu kuingia
eneo la machimbo.
Waziri Mkuu Pinda wakati wa maziko ya walioangukiwa na kufukiwa na
kifusi katika eneo hilo Machi 14 mwaka jana baada ya kazi ya kuwaopoa
kushindikana, alitoa siku 90 na kuwataka wachimbaji hao kusitisha
shughuli za uchimbaji katika eneo hilo na kwamba baada ya muda huo
serikali ingelitoa tamko lingine.
Pia Waziri mkuu aliagiza kujengwa kwa mnara na kuzungushiwa uzio
katika eneo hilo na hasa shimo ambalo wachimbaji hao walifukiwa na
hivyo serikali kuamua wazikwe ndani yake. Lakini kufikia jana, agizo
hilo lilikuwa halijatekelezwa.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Philemon Shelutete hakupatikana jana
kuzungumzia tukio hilo na kauli ya serikali kwa ujumla juu ya eneo
hilo, na hasa ikizingatiwa kwamba siku 90 zilizotolewa na Waziri Mkuu
kwa ajili ya wachimbaji hao kusitisha shughuli za uchimbaji katika eneo
hilo zimemalizika na sasa ni mwaka mmoja na siku 14.
Hadi tunakwenda mitamboni kulikuwa na taarifa kwamba serikali
ingelitoa tamko juu ya kuwepo kwa eneo hilo juu ya kuendelea kuchimbwa
ama la, kazi ambayo ilitarajiwa kufanywa na Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja Jijini mwanza.
Sunday, May 2, 2010
Dhahabu yamwaga damu
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Sunday, May 02, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment