Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Julai 19, 2014, saa 4:14 asubuhi
WASWAHILI wana msemo maarufu usemao`Utavuna
ulichopanda`. Kama ulipanda kokoto utavuna kokoto, usitarajie kuvuna mahindi.
Kwa muda mrefu sasa, timu ya Taifa ya Tanzania,
Taifa Stars imekuwa ikijiandaa kucheza mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu hatua
ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za AFCON mwakani nchini Mrocco
dhidi ya timu ya Taifa ya Msumbiji `Black Mambas`.
Mechi hiyo muhimu itachezwa kesho katika dimba la
Taifa, jijini Dar es salaam ambapo Stars
watahitaji kupata ushindi mkubwa ili kujiweka mazingira mazuri ya kusonga mbele
kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo mjini Maputo nchini
Msumbiji.
Stars iliweka kambi ya wiki mbili nchini Botswana
kwa lengo la kujiweka sawa na wakiwa huko walicheza mechi za majaribio ikiwemo
ile waliyofungwa mabao 4-2 dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo.
Baadaye ilirejea nchini na kwenda kuweka kambi
nyingine mjini Tukuyu, mkoani Mbeya na sasa timu ipo tayari kuivaa Mambas .
Safari hii Taifa Stars imeonekana kuwa na
maandalizi mazuri chini ya kocha Mart Nooij. Kwa haraka haraka, unaweza kusema
pengine inaweza kufanya makubwa na kuvuna walichopanda kwenye kambi mbili za
nje na ndani ya nchi.
Nooij amewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya
Msumbiji na aliifunga 1-0 Taifa Stars
mwaka 2007 katika dimba la Taifa kuwania kucheza fainali za mataifa ya Afrika,
mwaka 2008 nchini Ghana.
Kwa mazingira haya, Nooij anawajua wachezaji wa
Msumbiji na utamaduni wao. Na ndio maana jana alisema anao uwezo wa kuwafunga,
japokuwa alikiri kuwa mechi itakuwa ngumu.
Thomas Emmanuel Ulimwengu yuko fiti kuwaua Mambas kesho.
Wachezaji wote wako fiti kwa ajili ya mechi
isipokuwa kiungo wa Simba, Jonas Mkude kwani anasumbuliwa na maumivu ya goti na
kocha Nooij alisema atakuwa tayari kwenye mechi ya marudiano.
Wachezaji wa Stars wameonekana kuwa katika morali
kubwa ya kufanya vizuri ikizingatiwa wenzao wanaocheza soka la kulipwa nje ya
nchi wamewasili mapema tofauti na siku za nyuma.
Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao mara
nyingi wanapata utata wa kuruhusiwa na TP Mazembe ya DR Congo, safari hii
wametia miguu nchini mapema wakitokea nchini Tunisia ambapo timu yao imeweka
kambi ya kujiandaa na ligi ya mabingwa.
Mwinyi Kazimoto Mwitula anayecheza nchini Qatar naye
yupo nchini akiwa fiti. Wachezaji hao watatu, wamesema wapo tayari kwa mechi na
watapigana kufa na kupona kuisaidia timu yao.
Maandiliizi ya Stars yanaridhisha kwa kiwango fulani,
na inaonesha jinsi gani TFF ya Rais Jamal Malinzi imedhamiria kuwatoa Msumbiji.
Hili ni jambo jema, wamepanda mbegu nzuri na
matunda mazuri yanaweza kuonekana siku ya kesho.
Lakini maandalizi haya ya Stars hayafuti kauli
kuwa mpira wa miguu una matokeo matatu. Kuna kufunga, kufungwa na kutoa suluhu
au sare.
Wachezaji wamejiandaa kadiri wawezavyo na
watacheza kadiri wawezavyo ili kupata matokeo mazuri. Nao Msumbiji wana haki ya
kimpira ya kushinda. Timu yoyote inaweza kupata ushindi kutegemeana na mipango.
Taifa stars ipo nyumbani na ina faida kubwa.
Itakuwa na mashabiki wengi, ipo uwanja wake uliouzoea, kwahiyo wanayo mazingira
mazuri kuliko Msumbiji.
Mbwana Ally Samata alisema safari hii yupo fiti kuwavaa Mambas.
Lakini Msumbiji wanayo historia ya kuifunga Stars
katika mchezo wa mashindano ndani ya dimba la nyumbani. Hivyo tahahadhari kubwa
inatakiwa kuchukuliwa.
Waliokuwa na majukumu ya kuiandaa timu wamefanya
kazi yao, kesho ni zamu ya wachezaji kulipa maandalizi hayo.
Nao mashabiki sehemu yao ipo, wanatakiwa
kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu, kwasababu mashabiki ni mchezaji wa 12
uwanjani.
Watanzania kwa ujumla wao wanatakiwa kukaa nyuma
ya wachezaji ili kuwatia moyo. Tabia ya kuwazomea wanapokosea, kutawafanya
washindwe kuonesha kile walichokifuata Botswana na Tukuyu.
Kwa kikosi ambacho Nooij alitangaza kukiteua kwa
ajili ya mchezo wa kesho, kuna uwezekano wa kupata matokea.
Kipa yeyoye atakayeanza kati ya Deogratius Munish
`Dida` au kinda Aisha Manula anaweza kufanya vizuri, japokuwa Dida ana asilimia
kubwa ya kuanza kesho.
Mabeki ambao Nooij ataweza kuwatumia na wako fiti
kabisa ni Said Mourad, Ndir Haroub `Cannavaro`, Agrey Morris, Kevin Yondani na
Edward Charles.
Viungo ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Shaaban
Nditi, Simon Msuva, Himid Mao Mkami, Mwinyi Kazimoto, Khamis Mcha `Vialli`,
Ramadhani Singano `Messi`, Haroun Chanongo na Amri Kiemba.
Washambuliaji ni Mrisho Khalfani Ngassa, Thomas
Emmanuel Ulimwengu, Mbwana Ally Samatta na John Bocco `Adebayor”.
Kwa kikosi hiki, kuna kitu kinaweza kuonekana
kesho uwanja wa Taifa.
Kila la kheri Taifa Stars katika mchezo wa kesho.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa stars.
0 comments:
Post a Comment