Serikali
imewataka wananchi kuwatumia wasaidizi wa kisheria (paralegals) katika
kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria wanayokabiliana nayo na kuepuka
kupeleka mahakamani migogoro ambayo inaweza kusuluhishwa nje ya
Mahakama.
Wasaidizi
wa kisheria ni watu ambao hawana sifa za kuwa mawakili lakini kutokana
na uzoefu na ujuzi wao wanaweza kufanya kazi za usaidizi wa kisheria na
hivyo kushiriki katika kutatua migogogoro mbalimbali katika jamii.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Julai 18, 2014), Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria Mheshimiwa Angellah Jamsine Kairuki amesema kwa kufanya
hivyo, wananchi watakuwa wanashiriki moja kwa moja katika kupunguza
mlundikano wa mashauri mahakamani.
“Nichukue
fursa hii kuwasihi wananchi wanaokabiliwa na migogoro mbalimbali
kuwatumia vyema wasaidizi wa kisheria katika utatuzi wa migogoro,”
amesema Naibu Waziri Kairuki katika mkutano wake wa majumuisho ya ziara
ya siku tano jijini Dar es Salaam ambapo alizitembelea taasisi 13
zinazotoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.
Taasisi
hizo alizotembelea Naibu Waziri Kairuki ni pamoja na Chama cha
Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Envirocare, Kamati ya Msaada wa
Kisheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-LAC), Taasisi ya Mafunzo
ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).
Taasisi
nyingine zilizotembelewa ni Kituo kinachoshughulikia Maslahi ya
Wanawake na Watoto (TWCWC), Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wajane na
Watoto (CWCA), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Kituo cha
Msaada wa Kisheria cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Nyumba ya
Amani na Ofisi ya Mfuko wa Huduma za Kisheria (LAF).
Mafanikio na changamoto
Katika
mkutano huo, Naibu Waziri Kairuki amesema ameshuhudia mafanikio mengi
katika ziara yake yakiwemo kuanzishwa kwa kada ya wasaidizi wa kisheria
ambao wanawafikia wananchi wengi kwa ukaribu katika maeneo yao na kuwapa
msaada wa kisheria.
“Wasadizi
hawa wameweza kutatua migogoro mingi katika jamii zetu bila kufikisha
nashauri mahakamani na hivyo kupunguza uwezekano wa mlundikano wa
mashauri mahakamani,’ amesema.
Ametaja
mafanikio mengine aliyokutana nayo kuwa ni pamoja na asasi hizo
kushiriki katika mapambano dhidi ya ukimwi, ukatili wa kijinsia na
kingono pamoja na baadhi ya taasisi kuanza kutumia huduma za kisasa
katika kutoa huduma zikiwemo simu za mkononi.
“Baadhi ya taasisi kama TAWLA wanatoa huduma kupitia namba0800751010 (Vodacom) na namba 110017 (TTCL) wakati WLA wanatoa huduma kupitia namba 0800780100 ….hii ni kazi nzuri,” amesema.
Kuhusu
changamoto alizokutana nazo katika ziara yake, Naibu Waziri Kairuki
amesema amepokea malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi mahakamani na
malalamiko ya rushwa katika vyombo vinavyojihusisha na utoaji wa haki.
Changamoto nyingine ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu nafasi
ya wasaidizi wa kisheria katika utatuzi wa migogoro.
Chombo cha mpito (LAS)
kuratibu utoaji msaada wa kisheria
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, kutokana na mchango mkubwa wa taasisi
zinazotoa msaada wa kisheria kwa wananchi, Serikali kwa kushirikiana na
Wadau wa Maendeleo imeunda chombo cha mpito kinachoratibu shughuli ya
utoaji huduma za msaada wa kisheria nchini kinachofahamika kama
Sekretariaeti ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid Secretariat).
“Kupitia
sekretarieti hii, wadau wanaotoa msaada wa kisheria wanapata ruzuku
kutoka Serikalini ili kuweza kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa
wananchi wasio na uwezo,” amesema Naibu Waziri Kairuki katika mkutano
uliohudhuriwa pia na Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti hiyo wakiwemo Dkt.
Hellen Kijo-Bisimba, Bi. Theodosia Muhulo na Bw. Gideon Mandes.
Naibu
Waziri ameongeza kuwa tangu Sekretarieti hiyo iundwe mwezi Agosti, 2012
hadi mwishoni mwaka wa fedha uliopita (Juni, 2014), Serikali na wadau wa
maendeleo walikuwa wametoa zaidi ya Tshs 1.55 bilioni kwa taasisi 20
zinazotoa huduma za msaada wa kisheria nchini.
“Na
kimsingi asilimia 97 ya fedha za kuendesha LAS zinatolewa na Serikali na
asilimia tatu inatoka kwa wafadhili,” amefafanua Naibu Waziri Kairuki
ambaye ni mwanasheria kitaaluma na kuongeza kuwa kutokana na uwezeshaji
huo, mafanikio kadhaa yamepatikana kama alivyoshuhudia katika ziara
yake.
Kairuki
ameongeza kuwa kupitia fedha hizi, Sekretarieti imeweza kuwafikia na
kutambua walipo watoa huduma za msaada wa kisheria na kuanzisha
kanzidata (database) inayoonyesha hudua wanazotoa na mahali walipo.
“Hii
ni hatua kubwa sana ikizangatiwa kuwa awali taasisi hizo zilitoa huduma
bila kutambuliwa au kutambuana jambo lililowanyima fursa ya
kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao,”
amsema.
Akiongea
katika mkutano huo, Kwa upande wake, Bi. Muhulo ambaye pia ni
Mkurugenzi wa WLAC ameipongeza ziara ya Naibu Waziri na kusema
imeboresha mahusiano baina ya watoa huduma za msaada wa kisheria na
Seriali na kusisitiza ushirikiano huo ni muhimu katika utoaji wa huduma
bora za kisheria.
Kwa
upande wake, Dkt. Kijo-Bisimba ambaye pia ni Mkurugenzi wa LHRC amesema
taasisi zinazotoa msaada wa kisheria kwa wananchi zimefurahishwa na
hatua ya Naibu Waziri Kairuki kuzitembelea, kukutana na watumishi na
wananchi wanaopata msaada wa kisheria badala ya kusikia huduma hizo
kupiti vyombo vya habari.
“Tumefurahishwa
sana na kututembelea…wengine wanasikia tu kutoka kwenye vyombo vya
habari lakini yeye ametembelea hadi sehemu tunazotoa huduma za msaada,”
amesema Dkt. Kijo-Bisimba na kushauri kuwa wakati umefika kwa kutungwa
kwa sheria itakayowatambua wasaidizi wa kisheria na kuratibu utendaji
wao kwa manufaa ya wananchi.
Akizungumza
katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na
Sheria, Bw. Mandes ambaye pia Wakili wa Kujitegemea ameishukuru Serikali
kwa kuonyesha utayari wa kutunga sheria itakayoratibu wasaidizi wa
kisheria (paralegals) na kushauri kuongezwa kwa kasi ili sheria hiyo
ipatikane haraka.
Akifafanua
kuhusu utungwaji wa sheria itakayoratibu wasaidizi wa sheria, Naibu
Waziri amesema maandalizi ya kutungwa kwa sheria hiyo yamefikia hatua
nzuri Serikalini kabla ya kupelekwa bungeni.
0 comments:
Post a Comment