Dar es Salaam. Wakati
ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika
Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika
Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la
Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na
sakata hilo.
Kukamatwa
kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini
kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya IMTU.
Alisema
tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Bonde la Mbweni Mpiji ambako
iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu.
Kutokana
na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi saba likiongozwa na
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa
jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo.
“Katika
uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya binadamu vilitolewa
katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa
ajili ya kutupwa eneo la Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.
Alisema
mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo
vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina
mbalimbali.
“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema
katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika hospitali kama glovu,
nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema
jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kujua sheria gani
imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo na kwa nini wasitumie
utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna makosa ya kisheria,
hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Muhimbili wapokea mabaki
Meneja
Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo
imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya binadamu na kuhifadhiwa
wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni suala la polisi, ninachoweza
kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.”
Chanzo
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment