Msemaji wa Wakala wa Huduma za ajira (TaESA) bw. Peter
Ugata (katikati) akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu
mafanikio yaliyofikiwa na wakala huo ikiwemo kuanzisha ofisi za Kanda katika
Mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Mwanza na Arusha ili kusogeza huduma kwa
wananchi. Kulia ni Mratibu wa Huduma za Ajira toka wakala huo Bw. Joseph Haule
na Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bi Fatma Salum.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Wakala
wa Huduma za ajira (TaESA) uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari
Maelezo jijini Dar es salaam leo. Picha zote na Frank Mvungi, MAELEZO
**************************************
Frank Mvungi-Maelezo
Wakala wa huduma za ajira (TaESA) imefanikiwa
kuanzisha Ofisi za Kanda katika Mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Mwanza na
Arusha ili kusogeza huduma zake karibu na wananchi.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa wakala wa Huduma za ajira
Bw. Peter Ugata wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam.
Akifafanua Ugata amesema kuwa wakala imefanikiwa
kuanzisha ofisi katika mikoa hiyo ikiwa ni moja ya hatua za kuboresha huduma
zinazotolewa na wakala huo hapa nchini.
Akieleza zaidi Ugata alisema kuwa wakala huo
umeshawahudumia jumla ya wateja 14,608 kati yao wanaotafuta kazi ni 13,531
waajiri 993 na wakala binafsi zilikuwa 84.
Kwa upande wa kusajili fursa za kazi Ugata alisema
wakala umesajili fursa za kazi 3,143 kwa kutembelea waajiri 993 katika Mikoa ya
Shinyanga, Kagera, Mara, Mwanza, Singida, Tabora, Iringa, Morogoro, Lindi, Arusha,
Kilimanjaro na Mtwara.
Katika kuboresha huduma zake, Ugata amesema kuwa wakala
uko katika hatua za awali za kuweka mfumo wa kiteknolojia utakaowezesha
kukusanya na kusambaza taarifa za soko la ajira.
Katika hatua nyingine Ugata amesema wakala kupitia
kitengo cha kuwaunganisha watafutakazi 2,614na waajiri nje ya nchi za nje kama
Ujerumani, Brazil, China, Saudi Arabia, Denmark, India na Oman.
Katika kuhamasisha wananchi kutumia huduma za wakala
huo, Ugata amesema kuwa wakala umeweka utaratibu madhubuti wa kuratibu na
kusimamia uunganishaji wa watanzania kwenye soko la ajira nje ya nchi ili
wapate kazi zenye staha na kuepukana na biashara haramu ya usafirishaji watu (Human
Traffiking).
Wakala wa huduma za Ajira (TaESA) unatekeleza Sera ya
Taifa ya ajira ya mwaka 2008 na Sheria ya kukuza Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 na
katika hatua ya kukidhi matakwa ya Azimio NA.88 la mwaka 1948 la shirika la
kazi Duniani (ILO) ambalo Tanzania imeridhia.