Polisi akilinda Kituo cha Kupigia Kura
cha Shule ya Chekechea ya Mchwivila katika Jimbo la Kalenga, Iringa
jana . Picha na Edwin Mjwahuzi.
Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la
Kalenga, mkoani Iringa ulimalizika mwishoni mwa wiki na Chama cha
Mapinduzi (CCM), kiliibuka mshindi. Uchaguzi huo ulikuwa wa kuziba
nafasi iliyoachwa wazi na Dk. William Mgimwa aliyefariki dunia Januari
mwaka huu. Tunaipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuendesha
uchaguzi ulio huru na haki. Pamoja na kujitokeza kasoro ndogondogo za
hapa na pale, tume hiyo ilisimamia na kuendesha uchaguzi huo kikamilifu
na kutoa haki kwa vyama vilivyoshiriki pasipo kupindisha sheria.
Huu ni utamaduni mpya katika nchi
yetu, kwani sote ni mashahidi wa jinsi chaguzi mbalimbali zilizofanyika
huko nyuma zilivyokuwa zikiendeshwa kwa mizengwe. NEC ilikuwa ikikiuka
waziwazi kanuni na sheria za uchaguzi, hasa kutokana na shinikizo kutoka
kwa wanasiasa na baadhi ya viongozi serikalini. Vyombo vya ulinzi na
usalama navyo vilichangia kuwapo kwa kasoro nyingi katika chaguzi hizo
kutokana na kuegemea upande mmoja na kukandamiza upande wa pili.
Wakati tukiipongeza Tume hiyo kwa
kuendesha na kusimamia uchaguzi huo vizuri, hatuna budi kulaani vitendo
vya kihuni na kiharamia vilivyofanywa na kikosi cha ulinzi cha CCM
kinachojulikana kama Green Guards. Katika tukio linalopaswa kulaaniwa
kwa nguvu zote na wapenda amani wote pasipo kujali misimamo yao ya
kisiasa, walinzi wa kikosi hicho walimteka, kumtesa na kumdhalilisha
mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili wa Chadema ndani ya ofisi za CCM
mkoani Iringa kwa madai ya kumkuta akitoa rushwa, huku yeye akisema
alikuwa akitoa maelekezo kwa mawakala wa chama chake.
Mbunge huyo sasa amelazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Katika tukio hilo, polisi
wanadaiwa kumgeuzia kibao na kumfungulia mashtaka badala ya kuwakamata
makada hao wa CCM waliomteka na kumtesa kwa tuhuma za kutunga. Pia
katika tukio la awali, walinzi hao wanadaiwa kumteka na kumtesa padre wa
Kanisa la Orthodox katika Parokia ya Nyamihu, Costantino Mbilinyi kwa
kumhusisha na kampeni za moja ya vyama vya siasa vilivyokuwa vikishiriki
katika kinyang'anyiro hicho.
Hakuna asiyejua kwamba kujichukulia
sheria mkononi ni kosa la jinai. Jukumu la kila mwananchi ni kutoa
ripoti polisi au katika vyombo vingine vya ulinzi na usalama pale
anapomwona mtu yeyote akitenda kosa. Kama walinzi wa kikosi cha Green
Guards cha CCM walimkuta mbunge huyo akitoa rushwa walipaswa kutoa
ripoti polisi na kutoa ushahidi badala ya kumteka, kumpeleka katika
ofisi za chama hicho kumtesa na kumdhalilisha. Kama kweli walikuwa na
nia njema, kwa nini walishindwa kutoa ripoti Takukuru ambacho ndicho
hasa chombo kinachohusika na kupambana na vitendo vya rushwa?
Tumekuwa tukisema kwamba vikosi vya
ulinzi vya baadhi ya vyama vya siasa vya Green Guards, Blue Guards na
Red Brigades vinafanya vitendo vya jinai, hivyo vipigwe marufuku ili
kuinusuru nchi yetu na vita au balaa zozote zinazoweza kuchochewa na
vikosi hivyo. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anasema
anatafuta dawa ya kukomesha vurugu zinazojitokeza mara kwa mara katika
chaguzi zinazofanyika sehemu mbalimbali nchini. Hilo ni wazo jema.
Tunamshauri aanze kwa kupiga marufuku vikosi hivyo vya mgambo vya vyama
vya siasa ili makosa yaliyojitokeza Kalenga yasijirudie katika uchaguzi
wa Jimbo la Chalinze utakaofanyika mwezi ujao.
Chanzo, mwananchi