RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya Mrisho Kikwete
ameipa klabu
ya Simba Sh 30 milioni kwa ajili ya kukomboa hati yao ya kiwanja cha
Bunju B, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliwaambia wanachama wa klabu hiyo
jana Jumapili katika mkutano wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika
Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Rage alisema kwamba Rais Kikwete ametoa fedha hizo baada ya kufurahishwa
na umoja ulionyeshwa na baadhi ya wanachama wa Simba waliojitolea
kwenda katika uwanja huo kwa siku za karibuni na kufyeka majani na
kuonyesha kuwa wanauhitaji.
Rage alisema alikutana na Rais Kikwete saa 2 asubuhi jana Jumapili kabla
ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Simba na kumtakia heri katika mkutano
huo huku pia akitoa hundi ya Sh 30 milioni kwa ajili ya uwanja huo.
“Asubuhi leo saa 2 nilipata bahati ya kukutana na Rais Kikwete na
kututakia heri katika mkutano wetu na kama unavyojua kulikuwa na
matatizo ya kupata hati ya ardhi kule Bunju, tulikuwa tunadaiwa Sh 85
milioni, tulitoa milioni 50 hivyo nikamuomba Rais aingilie kati jambo
hili ili kuweza kupata hati mapema na kuanza ujenzi.”
“Rais akanikabidhi hundi ya milioni 30 kama mchango wake kwetu,
amedhihirisha ni mwanamichezo na mpenzi wa timu zote, kutokana na jambo
hilo naamini mambo yatakwenda vizuri na zile siku 100 alizotoa katibu wa
Simba kuwa baadhi ya vitu vitakuwa vimekamilika basi vitakamilika
kweli maana hadi kufikia siku hizo tutakuwa hata na sehemu ya kufanyia
mazoezi timu yetu,” alisema Rage.
Aliongeza: “Kikubwa alichofurahishwa ni juhudi za wanachama kwenda kule
na kuonyesha uhitaji wa uwanja na ndio maana akaamua kutoa fedha hizo
ili kuhakikisha tunapata hati ya ardhi na kuanza ujenzi mara moja.”
SOURCE: MWANASPOTI