Mmoja wa wananchi akichangia damu huku akisaidiwa na daktari.
MTANDAO
wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama (White Ribbon Allience for Safe
Motherhood) umekemea vikali tabia zinazofanywa na baadhi ya watumishi wa
hospitali na vituo vya afya ya kuuza damu ambayo kimsingi inatakiwa
kutolewa bure kwa wahitaji. Kauli hiyo ya pamoja imetolewa jana wilayani
Nkasi na wanaharakati wa mtandao huo walipokuwa katika hafla ya
uzinduzi wa wiki ya Utepe Mweupe wilayani hapa, mkoani Rukwa.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ‘Evidence for
Action’ ambao wanatekeleza mradi ujulikanao kama ‘Mama Ye’, Craig John,
alisema wamepata malalamiko toka kwa wananchi ya kuwa kuna tabia ya
baadhi ya watendaji kwenye sehemu za kutolea huduma za afya huwauzia
wagonjwa damu kitu ambacho hakikubaliki.
“…Wakati
tunapita pita mitaani kuhamasisha wananchi kuja kujitolea damu kwa
ajili ya akinamama wajawazito wanaohitaji kuongezewa damu, wananchi
walituambia kuwa baadhi ya watendaji wa afya wamekuwa kero kwao kwani
wanawauzia damu pindi wanapokuwa wanaihitaji,” alisema Craig.
Naye
Mratibu wa Utepe Mweupe nchini, Bi. Rose Mlay aliitaka serikali kutenga
bajeti mahususi katika mwaka wa fedha 2014/2015 ili kuhakikisha vituo
vya afya wanatoa huduma za dharura ikiwemo upasuaji na damu salama.
“…kama
mtoto amekaa vibaya tumboni kwa mama au hata kama amepigwa mwanamke
huyu anaweza kusaidiwa kwa kufanyiwa upasuaji na kuongezewa damu salama
pekee, hivi ndivyo vitakavyo muokoa,” alisema Rose.
Sherehe
za kilele cha Wiki ya Utepe Mweupe zinatarajiwa kufanyika Machi 15,
2014 wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa
kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.
0 comments:
Post a Comment