Wawakilishi wa Chama cha Uhifadhi wa Wanyama cha Frankfurt (FZS), wakikabidhi magari zaidi ya 11 kwa Rais Jakaya Kikwete Ikulu Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kusaidia vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori katika hifadhi na mbuga za taifa.Picha na Ikulu
====*******====
Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imenuia kumaliza kabisa ujangili nchini, ikiwa ni hatua ya kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka katika hifadhi za taifa.
Hakusita kusisitiza kwamba, nia ya dhati ya Serikali ni kuhakikisha mkakati huo unakamilika, japokuwa kumekuwa na changamoto zinazotokana na ukubwa wa hifadhi hizo na uhaba wa vitendea kazi pamoja na askari wa wanyamapori.
Akizungumza wakati wa kupokea magari 11 ya kisasa kwa ajili ya kusaidia operesheni ya kupambana na ujangili kutoka kwa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani, Kikwete alisema tatizo hilo limekuwa la muda mrefu, lakini juhudi za kulikomesha zinafanyika.
Alisema, pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, bado kuna tatizo la uhaba mkubwa wa wafanyakazi wanaotakiwa kudhibiti majangili, ambapo kwa sasa kuna wafanyakazi 1,155 sawa na asilimia 24 tu ya mahitaji halisi ya wafanyakazi 4,000 wanaohitajika.
"Mwaka uliopita, Serikali ilisimamia ajira ya wafanyakazi 449 na sasa kuna ajira ya wafanyakazi 500.
Kwa maana hiyo tutafikisha wafanyakazi
wapya 949 na kufanya mahitaji ya wafanyakazi wapya kuwa 4,000 zaidi ili
kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa viwango vya kimataifa," alisema.
Kwa mujibu wa viwango vilivyopo sasa,
mfanyakazi mmoja anasimamia eneo la kilometa za mraba 169 ikilinganishwa
na viwango vya kimataifa vya kilometa za mraba 25 kwa kila mfanyakazi
mmoja.
Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali
itaendelea kuajiri idadi hiyo ya wafanyakazi kila mwaka kwa miaka
mitatu ijayo ili kuhakikisha pengo lililopo linazibwa.
Alisisitiza kuwa, kampeni dhidi ya
ujangili ni suala la kimataifa na Tanzania au nchi zilizoathirika
hazitaweza kulikabili bila ushirikiano wa kimataifa.
Alisema upo ulazima wa kuteketeza
mitandao yote ya ujangili na kuwawajibisha ipasavyo watakaonaswa, kwani
kwa kufanya hivyo kutasaidia kulinda urithi huo wa dunia.
Ukosefu wa vifaa
Akifafanua, Rais Kikwete alisema
kuongeza idadi hiyo ya wafanyakazi pekee haitakuwa na maana iwapo
hawatakuwa na vifaa maalumu vya kisasa vitakavyowawezesha kukabiliana
ipasavyo na tishio la ujangili.
Katika mkakati wa maboresho hayo,
Kikwete alisema wanafanya jitihada za kuongeza idadi ya magari, kuongeza
vifaa vya kisasa kwa ajili ya doria na vifaa vya mawasiliano, ambavyo
vinahitaji uwezo mkubwa wa kifedha ambao utaweza kutekelezwa na serikali
kwa kipindi kirefu iwapo haitapata msaada wa uwezeshaji kutoka kwa
wadau.
Msimamo wa Wizara
Akizungumzia msimamo na mikakati ya
Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Lazaro Nyalandu alisema kutokana
na ukubwa wa tatizo, wanahitaji vifaa vya kisasa zaidi, ikiwamo
helikopta na ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufanya doria kwenye
maeneo yote ya mbuga na hifadhi za taifa.
Aliwatahadharisha wafugaji wanaopenda
kuingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi, akiwataka kuondoa mifugo
yao mapema kwa kuwa katika operesheni hiyo hakuna atakayeachwa.
"Katika operesheni hii, hakuna jangili wala mfugaji atakayeachwa iwapo atakutwa kwenye maeneo ya hifadhi," alisema.
Alifafanua kwamba, msaada huo wa
magari utapelekwa maeneo tofauti, matano kanda nane za Selous, mengine
matano Hifadhi ya Serengeti na moja Hifadhi ya Maswa.
Mwaliko wa vyombo vya habari
Nyalandu alisema Wizara yake
imevialika vyombo vyote vya habari vya kimataifa kwa ajili ya kuja
kupata taarifa sahihi kuhusu kampeni dhidi ya ujangili zinavyotekelezwa
ili kuepuka ripoti za upande mmoja kwa ajili ya kuweka usawa.
Alisema hatua hiyo ilichukuliwa na
wizara yake walipokwenda kwenye mkutano maalumu na Rais Kikwete
ulioandaliwa na mtoto wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles kwa ajili
ya kuangalia namna ya kulinda wanyama walio hatarini kutoweka duniani,
wakiwemo tembo na faru.(P.T)
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment