Mwenyekiti wa MCT, Kajubi Mukajanga
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema halijaupokea vizuri uteuzi wa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia kwani linamuona kama ni mpinzani wa tasnia ya habari nchini.
Hata hivyo, MCT limesema halimwingilii
Rais Jakaya Kikwete kwa maamuzi yake kwani huwateua anaowaona wanafaa
kwa sababu ni wasaidizi wake kulingana na malengo aliyonayo. Akizungumza
na NIPASHE jana Mwenyekiti wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema uteuzi
wake umelisikitisha baraza hilo kwani Nkamia ni mtu asiye na nia njema
na vyombo vya habari kulingana na matamshi yake bungeni na kwingineko.
"Tunatambua kazi ya uteuzi ni ya rais
na hatumwingilii katika hili, lakini sisi kwa uteuzi wa Nkamia tunaona
kama ni meseji ambayo Rais anatutumia ambayo si nzuri sana kumteua mtu
asiye na nia njema na vyombo vya habari kuwa katika wizara hii," alisema
Mukajanga.
Alisema ni ngumu kufanya kazi na
Nkamia kwa sababu ya msimamo wake wa kupinga uhuru wa vyombo vya habari
na pia uelewa wake kuhusu dhana ya vyombo vya habari kujisimamia
vyenyewe na dhana ya utangazaji kwa ajili ya umma.
Mukajanga aliongeza kuwa MCT itaendelea kufanya kazi na serikali.
Lakini alisema pia kuwa baraza litaendelea kuhimiza upatikanaji na usimamizi wa sera na sheria za vyombo vya habari.
Lakini alisema pia kuwa baraza litaendelea kuhimiza upatikanaji na usimamizi wa sera na sheria za vyombo vya habari.
Naye George Mbara, mkazi wa Dodoma
alisema ameshangazwa na uteuzi wa Nkamia. "Siku zote bungeni Nkamia
hakuwahi kutetea vyombo vya habari na siku zote amekuwa akiponda
waandishi wa habari, Jukwaa la Wahariri na MCT akiziita kuwa ni taasisi
ambazo hazina faida...leo hii ataongozaje taasisi ambazo amekuwa
akizidharau?" alihoji.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment