Msemaji wa Serikali ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene akiwaonyesha waandishi
wa habari jana mjini Dar es salaam kichwa cha habari cha gazeti la
“Malawi News” kinachosemeka “MALAWIANS FACE XENOPHOBIA IN TZ” ambacho
kilichapishwa na gazeti hilo kuhusu madai ya kubaguliwa raia hao wa
kutoka Malawi jambo ambalo sio kweli.
Msemaji wa Serikali ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene akitoa ufanunuzi kwa
waandishi wa habari jana mjini Dar es salaam juu ya taarifa
zilizochapishwa na gazeti la Malawi News kuwa Wamalawi waishio nchini
Tanzania wanaogopa kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa na
Watanzania taarifa ambazo sio kweli.
---
Na Benedict Liwenga-MAELEZO-Dar es salaam
SERIKALI ya Tanzania imekanusha
taarifa zilizochapishwa na gazeti la nchini Malawi lijulikanalo kama
“Malawi News” kuwa Wamalawi waishio nchini Tanzania wamekuwa wakiogopa
kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa na Watanzania.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Assah Mwambene amesema kuwa
taarifa hizo ni za kupotosha umma na kuleta chuki dhidi ya Tanzania na
nchi jirani na hazina ukweli wowote ule.
Bw. Mwambene ameongeza kuwa hakuna raia yeyote wa kutoka Malawi aliyebakwa wala kunyanyaswa kwa namna moja ama nyingine.
“Hakuna mwananchi yoyote kutoka
Malawi aliyebakwa , wala hakuna raia yoyote wa Malawi aliyepo hapa
nchini anayeogopa kutoka nje kwa sababu ya ubaguzi wowote ” amesisitiza
Mkurugenzi huyo.
Amesema kuwa licha Tanzania
kuwakamata wahamiaji haramu 1030 kutoka Malawi, Serikali ya Tanzania
iliwapa fomu ili kama walikuwa wanahitaji kuishi nchini wahalalishe
uwepo wao hapa Tanzania kwa wale wote walionyesha nia ya kuendelea
kuwepo hapa nchini .
Aidha wahamiaji wote haramu 1030 kutoka Malawi waliachiwa huru na wanaendelea kukamilisha taratibu za kuhalalisha uwepo nchini.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa
mpaka sasa kati wahamiaji haramu 1030 hakuna aliyewekwa ndani ama
kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kosa la kuwepo kinyume.
Kufuatia taarifa hizo ,Mkurugenzi
huyo amelitaka gazeti hilo kusahihisha taarifa hiyo na kuiomba radhi
Tanzania kwa upotoshaji huo na kuongeza kuwa kauli hiyo ni sawa na
matusi kwa Tanzania.
Aidha amesema kuwa hadi hivi sasa
zaidi ya wahamiaji haramu 24,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokarisia ya
Kongo (DRC) , Rwanda, Burundi , Uganda na Zambia wamerejeshwa makwao kwa
kosa la kuishi Tanzania bila vibali.
0 comments:
Post a Comment