Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri amesema jana alipanga kufuta mazoezi ya jioni ili wachezaji wake wapate nafasi ya kushuhudia mechi ya Ligi Kuu ya England katika ya timu mbili za ‘Big Four’, Liverpool na Arsenal.
Simba iko kambini mjini Zanzibar ikijiandaa na mechi yake ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana kutoka kambini kwao mjini Zanzibar, Phiri alisema ameamua kufanya hivyo ikiwa ni kama sehemu ya kujifunza katika kufanya maandalizi ya mechi yao Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga, keshokutwa lakini pia maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa ujumla.
“Tunahitaji kutoka kambini na kwenda sehemu kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo, nimewasilisha ombi hilo kwa uongozi ili jioni tusifanye mazoezi na kwenda kuangalia mechi hiyo,” alisema Phiri shabiki mkubwa wa Manchester United.
“Soka la kisasa linabadilika kila kukicha, kila inapochezwa mechi moja hasa ya ligi zilizoendelea kama England, Hispania na kwingine Ulaya unajifunza mambo mengi sana. Ninaamini wachezaji wana uwezo wa kujifunza wakati wakiangalia.
“Tutafanya hivyo, tutatoka kambini na kwenda sehemu maalum kwa ajili ya kuangalia na baada ya hapo, Jumatatu (leo) tutaendelea na programu yetu kama kawaida.
Ila hata hiyo Jumapili tutaendelea na programu ya mazoezi kama kawaida,” alisema Phiri baba wa watoto wawili. Kuhusu maandalizi ya mechi hiyo, Phiri alisema yanaendelea vizuri huku akisisitiza kuwa, zinapokutana timu hizo hakuna suala la sawa na mechi ya kirafiki.
“Lazima kufanya maandalizi ya kutosha, ni mechi iliyojaa mambo mengi ya siasa za soka. Kitu kizuri ni kushinda na ndicho tunachotaka kufanya. Tukishinda ndiyo suala zuri,” alisema Phiri aliyeiongoza Simba msimu uliopita kucheza mechi zote bila ya kupoteza hata mechi moja.
Wakati Yanga iko Bagamoyo, Simba imejichimbia kambini Zanzibar ikijiandaa na mechi hiyo na tayari imecheza mechi mbili za kirafiki na kutoka zote sare ya bila kufungana. Ilianza na Azam FC na Express FC ya Uganda.
0 comments:
Post a Comment