SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, August 16, 2010

Papic afungia wachezaji Yanga

Huku ikionekana ni kupanda kwa joto la mechi ya watani wa jadi, Kocha Mkuu wa Yanga, Kosta Papic ametangaza kuwazuia wachezaji wake kuzungumza au kufanya mazungumzo na mtu yoyote kutoka nje ya kambi ya timu hiyo. Simba na Yanga zinashuka dimbani keshokutwa katika mechi ya Ngao ya Hisani itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kila timu imejichimbia kambini kuhakikisha inaanza msimu huu kwa Baraka ya ushindi. Awali Papic alitangaza kutokuwa na hofu yoyote na mechi hiyo akidai kuwa anaiona ni sawa na zile kama dhidi ya Mtibwa Sugar au JKT Ruvu, lakini sasa amekiri ni mechi muhimu na inayohitaji umakini zaidi. Akizungumza jana kutoka katika kambi ya timu hiyo mjini Bagamoyo, Pwani, Papic alisema amechukua uamuzi wa kuwafungia wachezaji wake kuzungumza na mtu yoyote kutoka nje ya kambi hiyo kwa mambo mawili makuu. “Kwanza kuhakikisha wachezaji wanakuwa makini na kuelekeza akili yao katika mechi hiyo dhidi ya Simba. Pili kuepuka masuala ya siasa za Yanga na Simba, ni mechi ya watani lakini imejaa siasa nyingi ambazo ninaamini usipokuwa makini zinakuvuruga,” alisema Papic raia wa Serbia aliyewahi kuzinoa Enyimba na Lobi Star za Nigeria. “Inaweza kuonekana ni kitu cha ajabu, lakini ninafanya hivyo kulingana na mazingira na mechi yenyewe. Kwetu ni mechi muhimu kama tutashinda, mimi ninaichukulia kama mechi nyingine tu lakini kama unacheza mechi dhidi ya washindani wakubwa kitu muhimu ni kushinda. “Hivyo nimeshawataarifu wachezaji kwamba, nimezuia suala mchezaji kuzungumza na mtu kutoka nje ya kambi, iwe ni mtu wa kawaida au mwandishi. Najua mtanielewa,” alisema na alipoulizwa kama amewapokonya simu, Papic kocha wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini aliongeza; “Simu zao wanazo, siwezi kufanya hivyo. Kwangu nimefungia ninayokueleza kambini lakini siwezi kuwachunga kufanya kila kitu. Yaliyobaki wanapaswa wafanye wao na kwa kuwa mpira unachezwa hadharani hakuna cha kuficha. Hii inatokea hata Ulaya lakini ni katika baadhi ya mechi, mfano mechi muhimu za Ligi ya Mabingwa Ulaya.” Kuhusu maandalizi, Papic alisema yanaendelea vizuri na wana imani watafanya vizuri katika mchezo wa keshokutwa ingawa alisisitiza. “Sidhani kama ni kambi nzuri sana na ninapata kila ninachotaka, lakini tunajitahidi kutumia mazingira na kila kitu tulichonacho ili kufanya vizuri.” Mara ya mwisho, Yanga ikiwa chini ya Papic ililala kwa Simba mabao 4-3 kwenye uwanja huo huo, hali inayomfanya kocha huyo kuhakikisha anaibuka katika mechi ya Jumatano na kulipa kisasi.
Na Saleh Ally

0 comments:

Post a Comment