Jamii ya watu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo wanaoishi nchini Uingereza wamezindua kampeni maalum mjini London,
iitwayo Congo Unite.
Lengo ni kuchangisha fedha ili kuwasaidia watu
wenye maradhi ya selimundu (sickle cell) na watoto walioachwa yatima
kutokana na maafa ya vita nchini Congo.
Kampeni hiyo imeanza kwa uzinduzi wa mkanda
maalum wa video na CD za wimbo maalum uitwao Congo Unite ulioimbwa kwa
kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa Congo wanaoishi nchini Uingereza.
Video hizo zitauzwa duniani kote kuchangisha
fedha kwa ajili ya kusaidia mpango huo.
Kampeni hii imepewa jina la Congo Unite ikiwa ni
wito kwa raia wote wa Congo duniani kusahau tofauti zao na kuungana na
kushirikiana kwa pamoja katika kujaribu kusaidia kutatua matatizo
mbalimbali yanayowakabili raia nchini humo.
Kampeni hii imeanza kwa kulenga kuwasaidia watu
wanaokabiliwa na ugonjwa wa selimundu, watoto yatima na matatizo mengine
yatokanayo na maafa ya vita.
Akizungumza na BBC mkurugenzi wa Masoko na
Uhusiano wa CONGO50 ambaye pia ndiye aliyeongoza utengenezaji wa video
hiyo ya Congo Unite amesema mbali na kutumia fedha zitakazopatikana
kutokana na mauzo ya CD na Video hizo kutumika kusaidia waathirika wa
selimundu, wanategemea pia kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima
nchini Congo.
Naye mratibu wa kampeni hiyo, Mimi Zabu
Litambola, amesema moja ya mambo yanayotiliwa mkazo ni kukusanya fedha
ili kutafsiri vitabu na maelezo kuhusu ugonjwa wa selimundu kutoka lugha
ya kiingereza kwenda katika lugha zote zinazutumika nchini Congo.
Hatua hiyo itaiwezesha jamii ya Congo kupata
elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huo.
Kampeni ya Congo Unite ni moja ya mipango
iliyoandaliwa na raia wa Congo nchini Uingereza katika kuadhimisha miaka
50 ya uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
0 comments:
Post a Comment