Soko la pamoja Afrika Mashariki laanza
Mataifa matano ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
yanajumuika rasmi katika ushirika mpya wa kiuchumi kwenye kanda hiyo.
Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania na Burundi
wanaunda soko la pamoja Julai mosi.
Rais Mwai Kibaki wa Kenya amesema ushirika huo
mpya ambao unachukuliwa kuwa hatua ya kwanza kufikia muungano wa kisiasa
utachangia kuongeza mitaji, kuleta ajira na kuimarisha uhuru wa
biashara na pia kufanya kazi bila kikwazo katika nchi yoyote mwanachama.
Huu ni mwendelezo uliotokana na kuwepo kwa mfumo
wa umoja wa forodha ulioanza miaka mitano iliyopita ambapo baadhi ya
bidhaa kutoka Kenya zinapoingia nchi wenzake wanachama zilikuwa
zikitozwa ushuru ambao ulipungua kila mwaka hadi kumalizika hapo 2010.
Ilhali bidhaa kama hizo kutoka mataifa hayo ya
Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi hazikutozwa ushuru zilipokuwa
zikiingizwa katika soko la Kenya.
Hatua ya soko la pamoja haihusu tu bidhaa bali
pia kulegezwa kwa masharti kwa usafiri wa watu na upatikanaji wa ajira
na huduma katika mataifa hayo matano, jambo linaloendelea kuzua
mijadala.
Mijadala mingi inaelezea hofu kuwa mataifa
yaliyo na uchumi mkubwa katika jumuiya hiyo kama vile Kenya huenda
yakafaidi zaidi hasa katika upatikanaji wa nafasi za kazi na fursa
nyinginezo za maendeleo.
Ili kuepusha hali kama hiyo kila mwanachama
alipewa fursa kuwa huru kuchagua sekta zipi za ajira zifunguliwe kwa
raia wa eneo hilo na kwa wakati gani ili kukidhi mahitaji ya nchi
husika.
Makubaliano hayo ni baadhi ya yaliyojadiliwa na
kufikia hatua ya kutia saini mkataba huo.
Kenya ndilo taifa lililotoa fursa nyingi ikiwa
ni ajira kutoka fani 96 ambao utekelezeji wake unaanza mwaka huu huku
wanachama wenzake wakitoa nafasi pungufu kwa mfano Uganda 46 , Rwanda
16, Tanzania 10, Burundi 6 na baadhi zitatekelezwa kufikia 2015.
Taratibu za uvukaji mipaka japo zimeboreshwa
hati za kusafiria bado ni lazima kutumika.
Kwa upande wa vibali vya kazi, yeyote kutoka
nchi wanachama hana haja ya kuwa navyo akitaka kutafuta kazi nchini
Kenya na Rwanda pekee.
0 comments:
Post a Comment