SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, July 15, 2010

Rais Museveni ataka majeshi zaidi Somalia

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
 KAMPALA
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameelezea haja ya kuimarishwa kwa majeshi ya Afrika ya kulinda amani nchini Somalia na kufikia wanajeshi elfu 20 ili kuwateketeza wale wote waliyohusika na mashambulio ya mabomu mjini Kampala ambapo watu zaidi ya 70 waliauawa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Ntungamo magharibi mwa Uganda, Rais Museveni amesema kuwa nchi yake inaweza kushiriki katika mpango huo wa kuwa na wanajeshi elfu 20 ambao watashirikiana na serikali ya mpito kuwateketeza magaidi.
Amesema mataifa ya Afrika Mashariki yamekubali kutuma wanajeshi wa ziada elfu mbili nchini Somalia, lakini baada ya tukio la Jumapili mjini Kampala,Rais Museveni amesema wanajeshi zaidi wanahitajika.
Kundi la Al Shaabab limedai kuhusika na shambulio hilo la mabomu na limetishia kufanya tena mashambulio kama hayo nchini Burundi.Burundi na Uganda ndiyo pekee zenye wanajeshi katika kikosi cha wanajeshi elfu sita cha Afrika cha kulinda amani nchini Somalia AMISOM.
Wakati huo huo kiongozi wa kundi la al-Shaabab Sheik Muktar Abu Zubayr amesema mashambulio hayo ya Uganda ni mwanzo tu na kwamba mashambulio zaidi yatafuatia.
*********************
Wakili mtetezi wa ICTR auawa Tanzania
Yussuf Munyakazi
Wakili mwandamizi wa utetezi nchini Tanzania wa mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoshughulikia kesi za washukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda amepigwa risasi na kufa nje ya nyumba yake mjini Dar es Salaam.
Profesa Jwani Mwaikusa, ambaye pia alikuwa mkufunzi katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, aliuawa wakati akitaka kuingia nyumbani kwake nje kidogo ya mji huo.
Polisi wanasema mpwa wake pamoja na jirani yake waliuawa pia.
Imearifiwa kuwa wahalifu hao walilipekua gari la marehemu na kuondoka na mkoba wake wa kazi pamoja na hati kadhaa.
Bw Mwaikusa alikuwa wakili mtetezi wa mfanyabiashara wa Rwanda Yussuf Munyakazi anayekabiliwa na tuhuma za kuhusika katika mauaji ya kimbari kwenye mahakama ya kimataifa mjini Arusha.
Wakati akimtetea, alifanikiwa kuzuia Munyakazi asirejeshwe nchini Rwanda, kwa hoja kuwa asingeweza kutendewa haki na mahakama za huko.
Gazeti la Citizen nchini Tanzania limesema kumekuwepo na ongezeko la matukio ya uhalifu mjini Dar es Salaam katika siku za hivi karibuni.
Watu watano wameuawa kwa risasi na wahalifu wenye silaha katika kipindi cha miezi mwili iliyopita.
bbc.co.uk/swahili/habari

0 comments:

Post a Comment