Emile Heskey atundika Viatu
Mshambuliaji wa timu ya soka ya
England Emile Heskey ametangaza kustaafu kutoka soka ya kimataifa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa
miongoni mwa kikosi kilichoongozwa na Fabio Capello huko Afrika ya
kusini hadi hatua ya pili ya fainali za Kombe la Dunia.
Mara ya kwanza kwa Heskey kuichezea timu ya
England ilikuwa mwaka 1999 dhidi ya Hungary na tangu hapo ameichezea
mara 62 akifunga magoli saba.
Kwa kauli yake binafsi mchezaji huyo anasema,
''Nimefurahia kila nilipoichezea timu ya Taifa langu kwa fahari na
furaha''
Nawashukuru viongozi wote wa timu hii
walioniwezesha kushiriki pamoja na mashabiki walioniunga mkono katika
kipindi chote nilipovaa jezi ya timu ya England.
Heskey alikuwa miongoni mwa timu ya England ya
mwaka 2002 iliyoshiriki Kombe la Dunia halikadhalika kushiriki michuano
ya Kombe la Mataifa ya Ulaya ya mwaka 2000 na 2004.
Aliweza kufunga bao kwenye mashindano ya mwaka
2002 dhidi ya Denmark lakini alishindwa kufunga bao lolote huko Afrika
ya kusini England ilipopambana na Marekani na Algeria kabla ya mchuano
dhidi ya Slovenia na kupoteza mechi ya Ujerumani.
Heskey alishiriki Kombe la Dunia mwaka huu huko
Afrika ya kusini licha ya kuwa na msimu usioridhisha kwa klabu yake ya
Aston Villa lakini kocha Capello alimuamini kufanya vyema akimuweka safu
ya ushambuliaji pamoja na Wayne Rooney.
Mashabiki wengi na wachambuzi wa soka
hawakukubaliana na uamuzi wa kocha kwa hoja kwamba licha ya umbo kubwa,
Heskey ameshindwa mara nyingi kutikisa nyavu za upinzani.
Pamoja na kwamba alisaidia kwa mgongeo
aliompitishia Steven Gerard katika sare ya 1 - 1 dhidi ya Marekani
alishindwa kumalizia alipobaki na kipa wa Marekani mpira ukaishia
miguuni mwa kipa.
Aliingia zikisalia dakika 19 za mchuano dhidi ya
Ujerumani wakati Ujerumani ikiongoza bao 3 - 1.
**************************
Thierry Henry astaafu soka ya kimataifa
Mchezaji mashuhuri wa timu ya
Taifa ya Ufaransa na Barcelona Thierry Henry ametangaza kustaafu soka ya
kimataifa na timu ya Taifa.
Henry mwenye umri wa miaka 32 ametangaza uamuzi
huo wakati wa mahojiano na shirika la habari AP kabla ya kufikia uamuzi
wa kujiunga na klabu ya mpira wa miguu ya New York Red Bulls.Amesema kuwa anajiunga na klabu ya Red Bulls nchini Marekani, siyo kwa kutaka kumuiga David Beckham kwa kusafiri mara kwa mara baina ya Ulaya na Marekani. Amesema huu ndiyo mwisho kwake kushiriki timu ya Taifa. Alitia fora wakati akichezea klabu ya Arsenal ambako alikuwa nahodha na anatazamiwa kushiriki pambano la Red Bulls dhidi ya mahasimu wakuu wa klabu yake ya zamani, Tottenham hotspurs hapo tarehe 22 Julai. Alipohama kutoka Arsenal mnamo mwaka 2007, Henry alijiunga na Barcelona ya Uhispania na alikuwa na mwaka mmoja uliosalia kwenye mkataba wake aliporuhusiwa na Barcelona kuweza kuihama. |
0 comments:
Post a Comment