Waliofanya njama za kumpindua Rais Jammeh wahukumiwa adhabu ya kifo
Jaji wa
Mahakama Kuu ya Gambia amewahukumu watu wanane akiwemo mkuu wa zamani wa
majeshi ya nchi hiyo adhabu ya kifo baada ya kupatikana na hatia ya
kupanga njama mwaka jana za kumpindua Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo.
Jaji Emmanuel Amadi amesema kuwa, watu hao wanaruhusiwa kukata rufaa
katika kipindi cha siku 30 zijazo. Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa
jeshi la Gambia kupanga njama za kumpindua Rais Jammeh. Rais Yahya
Jammeh aliingia madarakani mwaka 1994 akiwa afisa kijana wa jeshi la
nchi hiyo na alikuwa na cheo cha Luteni, na ameendelea kuiongoza nchi
hiyo ndogo iliyoko Magharibi mwa Afrika, baada ya kushinda vipindi
vitatu vya uchaguzi wa rais. Taarifa zinasema kuwa, Langtombong Tamba
mkuu wa zamani wa majeshi, Lamin Bo Badjie mkuu wa zamani wa upelelezi
na Modou Gaye msaidizi wa mkuu wa zamani wa jeshi la polisi nchini humo
ni miongoni mwa maafisa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya
kifo.
****************************
****************************
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kutembelea Uganda na Sudan |
Scott Gration
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa ameanza safari ya mzunguko
itakayomchukua muda wa wiki mbili kwa kuzitembelea nchi za Sudan na
Uganda kwa shabaha ya kuchunguza kwa karibu migogoro na machafuko
yaliyotokea hivi karibuni katika nchi hizo. Katika safari yake hiyo,
Gration anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa Umoja
wa Mataifa na Umoja wa Afrika nchini humo na hali kadhalika kushauriana
na wajumbe kutoka Russia, China Uingereza, Ufaransa na Norway walioko
nchini Sudan kuhusiana na migogoro ya Darfur na kusini mwa Sudan. Hali
kadhalika atakutana na viongozi wa chama tawala cha National Congress na
kile cha Sudan People's Liberation Movement SPLM kuhusiana na
uitishwaji wa kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mapema mwakani. Mjumbe
maalumu wa Umoja wa Mataifa ataitembelea Uganda na kujadili na viongozi
wa Kampala mikakati ya kuisaidia nchi hiyo katika kukabiliana na
mashambulizi ya makundi ya kigaidi, na mpango wa kutumwa askari zaidi
kikosi cha kulinda amani nchini Somalia. http://kiswahili.irib.ir/ |
0 comments:
Post a Comment