IKULU imewatoa wasiwasi wananchi kuhusu usalama wa Rais Jakaya
Kikwete na kuwahakikishia kuwa mkuu wa nchi yuko katika mikono ya watu
makini, salama na wazalendo wanaoifahamu kazi yao.
Hayo
yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu,
Salvatory Rweyemamu, wakati akifafanua kuhusu tukio la magari matano
yaliyokuwapo kwenye msafara wa Rais mkoani Kilimanjaro kupatwa na
hitilafu na kushindwa kuwaka wakati wa ziara yake wiki hii.
Akifafanua
kuhusu tukio hilo lililotokea Juni 8, mwaka huu, alisema sehemu ya
magari ambayo ilikuwa yatumike kwenye msafara huo, yakiwa katika
utaratibu wa maandalizi ya kumpokea Rais Kikwete katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), yalipelekwa katika kituo cha mafuta
cha Rafiki.
“Baada
ya kujazwa mafuta magari matatu kati ya hayo matano, yalikataa kuwaka,
baada ya kuona hivyo, uamuzi ulichukuliwa wa kutoyawasha kabisa yale
magari mengine mawili,” alisema Rweyemamu.
Hata
hivyo, alisema kituo kilichotumika ni moja ya vituo ambavyo vimekuwa
vinatumiwa kujaza mafuta ya magari ya Rais siku nyingi na kwamba uamuzi
wa kuyajazia mafuta magari hayo katika kituo hicho haukuwa wa kushtukiza
ama kubahatisha.
“Ukweli
ni kwamba uamuzi wa wapi pa kujaza mafuta magari ya Rais, si wa
madereva, bali huanzia ngazi za juu,” alifafanua.
Alisema
kinachofahamika ni kwamba wakati magari hayo yanaingia kujazwa mafuta
kituoni hapo, yalikuwa mazima, imara na salama kwa ajili ya kumpokea
Rais Kikwete aliyekuwa anatokea Dar es Salaam na kwamba tatizo lilianza
baada ya kujazwa mafuta hayo.
Hata
hivyo, Rweyemamu alisema pamoja na hitilafu hiyo, msafara wa Rais
ulipokelewa kama ilivyopangwa bila tatizo lolote kutokana na misafara ya
aina hiyo mara zote huwa na mipango mbadala ya usafiri yenye kiwango
cha juu cha usalama.
Alisema
magari yaliyopata hitilafu hayakutumika kabisa katika msafara huo kwa
kuwa yalikuwa yanasafishwa ambapo baada ya kusafishwa na kuwekewa mafuta
mengine, yaliwashwa na kuwaka na yapo safarini kurejea Dar es Salaam.
“Uchunguzi
wa tukio hili zima kwa sasa uko mikononi mwa vyombo vya usalama ikiwamo
Polisi na Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA) na
wakikamilisha uchunguzi wao, wananchi watajulishwa nini hasa kilitokea,”
alisema.
Alisema tukio hilo haliathiri kitu chochote katika ziara hiyo na
wala halikusababishwa na uzembe na kuhusu usalama wa Rais, hauna shaka
yoyote na uko mikononi mwa watu wa kuaminika.
0 comments:
Post a Comment