Japan imeishinda Cameroon bao 1-0 katika uwanja
wa Free State mjini Bloemfontein, mechi ya kundi la E kwenye michuano ya
Kombe la Dunia.
Bao la Japan lilifungwa na Keisuke Honda katika
dakika ya 38 kufuatia kizazaa kwenye lango la Cameroon.
Pasi iliyotolewa na kiungo wa Japan Daisuke
Matsui iliwazidi kimo Nocolas Nkoulou na Stephane Mbia , mpira
ukakaribia lango na hapo ndipo Honda ambaye anaichezea klabu ya CSKA
Moscow alipomalizia kwa kufunga bao.
Stephane Mbia alikaribia kusawazisha katika
kipindi cha pili lakini kwaju lake likagonga mwamba.
Mshambuliaji wa Cameroon alidhibitiwa na walinzi
wa Japan, na alifanya jaribio moja tu katika kipindi cha pili baada ya
kuichenga safu ya ulinzi, akatoa pasi kwake Choupo- Moting ambaye
alipaisha mpira.
Awali katika kundi hilo la E Uholanzi iliishinda
Denmark mabao 2-0 katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.
Denmark walijifunga bao la kwanza kupitia Simon
Paulson, naye mchezaji wa Klabu ya Liverpool Dirk Kuyt akaifungia
Uholanzi bao la pili.
Miongoni mwa timu 6 za Afrika zinazoshiriki
michuano hiyo ya Kombe la Dunia, hadi sasa ni Ghana tu waliopata ushindi
baada ya kuwafunga Serbia bao 1-0 siku ya Jumapili.
Afrika Kusini walitoka sare moja kwa moja na
Mexico katika mechi ya ufunguzi, Nigeria ikashindwa 1-0 na Argentina
ilhali Algeria wakafungwa 1-0 na Slovenia.
Siku ya Jumanne timu nyingine kutoka Afrika-
Ivory Coast itacheza dhidi ya Ureno, mechi ya kundi G,mjini Port
Elizabeth.
Bado hakuna uhakika wa mshambuliaji wa Ivory
Coast Didier Drogba kucheza, baada ya kupata jeraha kwenye mechi ya
kirafiki.
0 comments:
Post a Comment