Gyan Asamoah
akiachia mkwaju kutikisa nyavu za Marekani na kuipatia Ghana tiketi ya
kucheza robo fainali.
Black Stars imezidi kuibeba Afrika, baada ya
timu hiyo ya Afrika Magharibi kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia
nchini Afrika Kusini ilipoitandika Marekani mabao 2-1 katika uwanja wa
Royal Bafokeng, mjini Rustenburg.
Mechi hiyo iliingia muda wa ziada baada ya
kipindi cha kawaida kumalizika 1-1.
Wakishangiliwa na maelfu ya mashabiki
waliofurika uwanja huo, vijana wa Ghana walianza kwa kasi huku
wakionyesha mchezo wa hali ya juu na katika dakika ya nne ambapo
Kevin-Prince Boateng alipopenya safu ya ulinzi ya Marekani na kuipatia
Black Stars bao la kwanza.
Kipindi cha pili kilimalizika Ghana wakiongoza
1-0, na katika kipindi cha pili walilazimika kuimarisha safu ya ulinzi
baada ya Marekani kurejea na mwamko mpya, hasa mshambuliaji wao hodari
Landon Donovan.
Katika dakika ya 62 Jonathan Mensah alimwangusha
Clint Dempsey kwenye eneo la hatari na hapo mwamuzi kutoka Hungary,
Viktor Kassai akawapa Marekani penalti, ambayo Landon Donovan aliifunga,
na kusawazisha.
Muda wa nyongeza
Muda wa kawaida ulimalizika kwa matokeo hayo ya
1-1 na kulazimisha mechi kuingia muda wa ziada.
Dakika tatu tu baada ya muda wa ziada kuanza
Asamoah Gyan alihimili kumbo la mlinzi wa Marekani, Carlos Bocanegra, na
kuifikia pasi ndefu iliyotoka kwa Andre Ayew, na kusukuma mkwaju mkali
hadi kwenye nyavu za lango la Marekani.
Sasa Ghana inasubiri kucheza na Uruguay kwenye
robo fainali Ijumaa ijayo.
Uruguay ilikuwa ya kwanza kujiandikishia nafasi katika robo fainali baada ya kuifunga Korea Kusini mabao 2-1 kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay, mjini Port Elizabeth.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Uruguay
wakiongoza 1-0, lakini baada ya mapumziko Korea Kusini walionekana
kuimarika na kuzidisha mashambulizi yaliyozaa matunda katika dakika ya
68, wakati Lee Chung-Yong alipofunga kwa kichwa kufuatia mpira wa
adhabu.
0 comments:
Post a Comment