SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, October 7, 2015

MIKUTANO YA MWAKA YA KUNDI LA BENKI YA DUNIA NA SHIRIKA LA FEDHA LA KIMATAIFA YAANZA RASMI NCHINI LIMA LEO TAREHE 5/10/2015


Dr. Servacius Likwelile Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa serikali wa katikati akiwa pamoja na Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu kushoto na Bi. Natujwa Mwamba Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania kulia, wakiwa katika mkutano wa chombo kinachotoa mafunzo ya kusimamia mambo ya uchumi (MEFMI) nchini Peru – Lima. ( Picha na Eva Valerian, Peru – Lima).
MIKUTANO YA MWAKA YA KUNDI LA BENKI YA DUNIA NA SHIRIKA LA FEDHA LA KIMATAIFA YAANZA RASMI NCHINI LIMA LEO TAREHE 5/10/2015

Mikutano ya mwaka ya Bodi ya Magavana ya Shirika la fedha la Kimataifa na kundi la Benki ya Dunia kwa mwaka 2015 imeanza rasmi hapa mjini Lima –Peru na kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka nchi mbalimbali Duniani ambapo kilele chake kitakuwa tarehe 12 mwezi Octoba 2015.

Bodi ya Magavana wa Shirika la Fedha la kimataifa ( Mfuko) na Bodi ya Magavana wa kundi la Benki ( Benki ) kwa kawaida hukutana mara moja kwa mwaka kujadili kazi za Taasisi ambazo ziko chini yao. Mikutano hii ya mwaka huwa inafanyika mwishoni mwa mwezi Septemba na mwanzoni mwa mwezi Octoba. Mikutano hii hufanyika mjini Washington kwa miaka miwili mfululizo na kwa mwaka wa tatu hufanyika kwa nchi mwanachama ambaye  amepitishwa kutokanana na viwango vilivyowekwa.

Mikutano hii ya Bodi ya Magavana ilizinduliwa huko Savannah, Georgia, Amerika mwaka 1946 na ikaanza kufanyika mjini Washington DC mwaka huo huo.

Mikutano hii ya mwaka itaambatana pamoja na mikutano ya kimataifa ya kifedha, kamati za fedha, Kamati za maendeleo, kundi la nchi kumi, kundi la nchi ishirini na nne, na makundi mbalimbali ya nchi wanachama.

Aidha katika kuhitimisha mikutano hii, Shirika la fedha la kimataifa, kamati ya mambo ya fedha, Kamati ya maendeleo pamoja na makundi mengine watapata nafasi ya kuwasiliana na kutoa mapendekezo yao ya kipi kifanyike ili kuhakikisha mambo wanayojipangia yanatekelezwa.

Magavana watakitumia kipindi hiki  kwa kuzungumzia masuala ya kibiashara na
kushauriana. Bodi ya Magavana inatumia kipindi hiki  kufanya maamuzi ya ni vipi mambo ya Fedha ya kimataifa yanapaswa kuwa na kukubaliana kuhusu maazimio yao.

Mikutano ya mwaka inakuwa na mwenyekiti ambaye ni Gavana wa Benki na wa Mfuko, na uenyekiti huo unakuwa ni wa kupokezana kati ya wanachama kila mwaka. Kila baada ya miaka miwili inachagua Mkurugenzi mtendaji. Kila mwaka wanachama wapya wowote wanakaribishwa katika Benki na mfuko.

Kwa sababu Mikutano hii ya mwaka inakusanya idadi kubwa ya wanachama kutoka
nchi mbalimbali, Shirika la fedha la kimataifa na kundi la Benki ya Dunia inatoa nafasi ya kuwapatia ushauri mkubwa na mdogo, kwa mpangilio wa kuwa na utaratibu maalumu au kutokuwa na utaratibu maalumu alimradi hawavurugi mpangilio uliopo.

Semina mbali mbali zinafanyika na zinaendeshwa na wafanyakazi wanachama kwa waandishi wa habari. Aidha programu za Mikutano ya mwaka zimetengenezwa kwa kuzingatia matakwa ya sekta binafsi, wajumbe kutoka Serikalini na maafisa wakuu wa Mabenki na watumishi wa Mfuko.

Mikutano ya mwaka iliyofanyika  nje ya Amerika kuanzia mwaka 1947 hadi 2015.

Mwaka          Mahali
1947                London
1950                Paris
1952                Mexico City
1955                Istanbul
1958                New Delhi
1961                Vienna
1964                Tokyo
1967                Rio de Janeiro
1970                Copenhagen
1973                Nairobi
1976                Manila
1979                Belgrade
1982                Toronto
1985                Seoul
1988                Berlin
1991                Bangkok
1994                Madrid
1997                Hong Kong
2000                Prague
2003                Dubai
2006                Singapore
2009                Istanbul
2012                Tokyo
2015                Lima


Magavana wa mikutano hiyo ni Mawaziri wa fedha kutoka nchi mbalimbali, Magavana wa Benki kuu na Makatibu wakuu wa Wizara za fedha.

Mpaka sasa karibu nchi zote zimeshawasili katika mikutano hiyo na hali ya hewa ni mawingu na baridi kiasi.

Imetolewa na:
Ingiahedi Mduma
Msemaji Mkuu
Wizara ya Fedha
Lima - Peru
5/10/2015

0 comments:

Post a Comment