SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, June 24, 2015

MAHAKAMA YA TANZANIAYAENDELEA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA ZA HAKI

  Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania (wa kwanza kushoto), Bw. Waleed Malik, Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia (wa pili kushoto), Bi. Neema Ndunguru, Mkurugenzi wa Mazingira ya Biashara (PDB) pamoja na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia wakiwa meza kuu wakati wa Kikao cha majadiliano katika ya Mahakama na Wadau wa Jumuiya ya Wafanyabiashara kupata maoni juu ya maboresho ya huduma za Mahakama.
 Mmoja wa wadau walioshiriki katika warsha hiyo akitoa maoni yake katika majadiliano hayo.
 Washiriki wakiwa katika kazi za makundi wakitoa maoni juu ya Mpango Mkakati wa Mahakama wenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma zake.   
(Picha na Mary Gwera, Mahakama).

Na Mary Gwera
KATIKA mwendelezo wa maboresho ya utoaji wa huduma ya haki nchini, Mahakama ya Tanzania inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau pamoja na Washirika mbalimbali wa maendeleo ili kupata maoni yao juu ya uboreshaji wa huduma zake.

Akiongea na Waandishi wa Habari mapema jana, katika Warsha iliyoandaliwa na  Mahakama ikishirikisha Ugeni kutoka Benki ya Dunia na Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara kutoka, TRA, Umoja wa Taasisi za Kifedha,MOAT, TIRA, TCRA n.k iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam, Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania alisema Mahakama imekuwa katika mchakato wa maboresho na washirika mbalimbali wa Maendeleo na wadau wa utoaji haki ili kuboresha huduma zake.
“Mikakati hiyo ya maboresho ni sehemu ya mpango wa miaka mitano (5) ya maboresho ya Mahakama ambapo unaenda sambasamba na maboresho ya miundombinu ya majengo ya Mahakama, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) nk” Alisema Kattanga
Mtendaji alisema maoni yanayoendelea kutolewa na wadau mbalimbali wa Mahakama utasaidia kubadili mtazamo mbaya wa wananchi walionayo kuhusiana na Mahakama na hivyo kusaidia kujitathmini na kubadili mfumo wake wa utoaji wa huduma. 
Aliongeza kuwa maboresho hayo yataenda sambasamba na kubadili mfumo wa ushughulikiaji wa malalamiko kuhusiana na mashauri mbalimbali na kurahisisha taratibu mbalimbali za kisheria zitakazowezesha wananchi kupata urahisi katika ufunguaji wa mashauri.
Kwa upande wake, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu-Ethiopia, Mhe. Dkt. Menbere Tseha Tadesse, ambaye ni miongoni wa Wawakilishi kutoka Benki ya Dunia (World Bank), alisema kasi ya jitihada mbalimbali zilizowekwa na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha huduma zake inatia moyo.
Alisema ufanisi wa Mpango Mkakati wa Mahakama utategemea maoni ya wadau mbalimbali wa Mahakama ili kupata njia bora za kuboresha huduma zake kwa wananchi.
Naye, Bw. Henry Mwanyika, Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), alisema amefurahishwa na uamuzi uliofanywa na Mahakama wa kujitathmini utendaji wake ambao umekuwa shirikishi, akiongeza kuwa uamuzi huu utawezesha Mahakama kupata maoni ya wadau ya nini kifanyike katika kuboresha huduma zake kwa wananchi.
“Kwa kweli nimefurahishwa sana na uamuzi wa Mahakama wa kutushirikisha sisi wadau katika mpango wake wa maboresho na tunahaidi kushirikiana nao bega kwa bega katika jitihada hizo,” alieleza.

0 comments:

Post a Comment