SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, February 10, 2015

MTOTO WA MIAKA SITA ABAKWA AUAWA KWA KUNYONGWA WAKATI AKICHUMA MATUNDA PORINI-SINGIDA
MKAZI wa Kijiji cha Mayaka, Kata ya Minyughe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Samaha Mtawa (6) amekufa baada kubakwa na kunyongwa wakati akichuma matunda porini.
 

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi, Thobias Sedoyeka, mwili wa mtoto huyo ulionekana Februari 7 mwaka huu saa 12 asubuhi umbali wa mita 150 kutoka nyumbani kwao.
 
"Uchunguzi wa awali umebaini marehemu alifariki baada ya kubakwa, kunyongwa na kutupwa porini na mtuhumiwa aitwaye Ramadhani Omari (28), mkazi wa Maweni," alisema.
 
Aliongeza kuwa, uchunguzi huo pia umebaini mbinu ambayo ilitumiwa na mtuhumiwa ni kumvizia marehemu akiwa anachuma matunda hivyo alimkamata kwa nguvu na kumfanyia unyama huo.
 
Kamanda Sedoyeka alisema licha ya marehemu kupiga kelele na wananchi kukimbilia eneo hilo ili kumwokoa, walipofika walikuta tayari amefariki na mtuhumiwa kakimbia lakini alikamatwa baada ya saa mbili.
 
"Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa kwa upelelezi zaidi na baada ya kukamilika, atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili, mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari na baadaye kukabidhiwa ndugu zake," alisema.
 
Amewahadharisha wazazi na walezi wa watoto kutowaachia ovyo watoto wao na kucheza katika mazingira salama ili wasiweze kufanyiwa vitendo vya kikatili kama ubakaji na mauaji jambo ambalo linaleta simanzi na majonzi.
 
Wakati huo huo, wananchi mkoani humo wametakiwa kuchukua tahadhari juu ya makundi ya kigaidi yaliyoanza kuingia nchini, kujihusisha na vitendo vinavyoleta uvunjifu wa amani kwa jamii na Taifa.
 
Wito huo ulitolewa jana na Kamanda Sedoyeka baada ya kukamatwa baadhi ya watuhumiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini wakidaiwa kujihusisha na matukio ya ugaidi ukiwemo wa ulipuaji mabomu na mauaji ya raia.

KWA HISANI YA MALUNDE BLOGw

0 comments:

Post a Comment