SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Saturday, October 18, 2014

No retreat, No Surrender

Mashabiki wa timu ya Yanga wakishangilia jukwaani
YANGA ilimsajili Emmanuel Okwi msimu uliopita kwa lengo la kuboresha fowadi yake, lakini baadaye mchezaji huyo akatofautiana na timu hiyo na kufuata taratibu za kisheria akarejea kwenye timu yake ya zamani, Simba ambayo leo Jumamosi inacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Simba wakafurahia ujio wa mchezaji huyo kwa vile anacheza kwa mapenzi zaidi akiwa kwao, lakini wenzao wa Yanga bado wakawa na mawazo kutokana na maneno ya mitaani pamoja na mamilioni ya shilingi ambayo Okwi alizoa kiulaini.
Okwi baada ya kukamilisha usajili wake Simba akawaambia Yanga akisema: "Yanga msije uwanjani Oktoba 18." Kauli yake inamaanisha kwamba leo atawadhalilisha.
Straika Mbrazili Genilson Santos 'Jaja' aliposikia maneno yamezidi na watu wanambeza akaipiga Azam mabao mawili kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na ilikuwa kama anawauliza mashabiki akisema: "Okwi wa kazi gani?"
Kama hiyo haitoshi, Andrey Coutinho aliposikia makelele hayo akawaambia mashabiki wa Yanga kwa ishara kwamba mambo yake yataonekana uwanjani hazungumzi sana. Hayo ndiyo kati ya mambo yatakayonogesha mechi hiyo ambayo kila upande umekoki silaha zake na kutamka kwamba 'No Retreat, No Surrender' wakimaanisha kwamba 'Hakuna kujisalimisha wala kurudi nyuma' bali lazima kieleweke ndani ya dakika 90.
Yanga yenye Wabrazili wanne akiwamo Kocha Mkuu, Marcio Maximo inakutana kwa mara ya kwanza msimu huu na Simba ya kocha mwenye uwezo mkubwa wa kusoma na kudhibiti mchezo, Mzambia Patrick Phiri.
Maximo na Phiri wamewaambia mashabiki wa soka nchini waache nongwa, waelekee uwanjani kushuhudia soka la aina yake ambalo halijawahi kuonekana tangu msimu huu uanze.
YANGA
Mbali na mazoezi mengine, Yanga imekuwa na siku tano za programu maalumu ya maandalizi dhidi ya Simba ambazo zimekamilika jana Ijumaa.
Kikosi hicho kiliweka kambi eneo la Kunduchi katika hoteli ya Landamark na kufanyia mazoezi yake katika Uwanja wa Boko Veteran.
Kwa wiki nzima, Maximo amekuwa akicheza na akili za wachezaji wake kwa kufanya vikao visivyo rasmi ikiwa ni njia ya kuwatengeneza kisaikolojia, jambo ambalo limekuwa likiongeza ufanisi na kupandisha morali kwa kikosi hicho kilichoshika nafasi ya pili msimu uliopita.
Awali viongozi pamoja na mashabiki wa Yanga walikumbwa na taharuki baada ya nahodha wa timu, Nadir Haroub 'Cannavaro' kupata majeraha kwenye mechi kati ya Taifa Stars na Benin, lakini kwa sasa ameonekana kuimarika hasa baada ya kupata ruhusa ya kucheza kutoka kwa Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani.
Chanzo:Mwanaspoti

0 comments:

Post a Comment