HOTUBA
MGENI RASMI MHE. HAWA GHASIA, WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU TAMISEMI
WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA SABA WA WADAU WA LAPF KWENYE UKUMBI WA
MIKUTANO WA AICC JIJINI ARUSHA TAREHE 23/10/2014
Mhe.
Gaudensia Kabaka (mb),Waziri wa kazi na Ajira,
Mheshimiwa Prof Hassa Mlawa, Mwenyekiti wa Bodi ya LAPF
Mhe.Magesa
Mulongo,Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Naibu
Mawaziri mlioko hapa,
Makatibu
Wakuu
Waheshimiwa
Wabunge Mlioko hapa,
Mwenyekiti
wa Bodi ya LAPF,
Uongozi
wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii,
Wageni
waalikwa,
Mabibi
na Mabwani.
Napenda kumshukuru Mwenyezimungu
kwa kutujaalia afya njema na kutukutanisha sisi sote siku ya leo. Mheshimiwa mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa LAPF na Menejimenti kwa ujumla, napenda
kuwashukuru kwa kunikaribisha siku ya leo kuwa mgeni Rasimi katika mkutano huu.
Ni siku ya kipekee kwa Mfuko wa LAPF, kwani pamoja na kufanya mkutano wa saba
wa wadau,mfuko unatimiza Miaka sabini tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1944.
Ndugu
Wadau,
Historia tuliyoipata kuhusu
Mfuko huu inatuonesha wazi kuwa Tanzania inapiga hatua katika maendeleo ya
sekta ya Hifadhi ya Jamii. Sekta ya hifadhi ya Jamii inaongozwa na sera yetu ya
Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003. Sekta hii ni pana na ipo katika mifumo mikuu
miwili ambayo ni sekta iliyo rasmi na sekta hisiyo rasmi. Katika sekta rasmi
tunayo mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii kama LAPF, PSPF,NSSF,GEPF,PPF na hata
NHIF na taasisi nyinginezo za aina hii. Katika sekta hisiyo rasmi tunazo
taratibu nyingi mbalimbali, tangu Ngazi ya familia, koo, jamii katika vijiji na
mitaa kupitia vyombo kama vikoba na mifumo mingineyo, inayolenga kuifadhi na
kulinda utu na heshima ya binadamu ndani ya jamii yake. Hivyo basi, Mfuko wa
LAPF ni moja ya vyombo rasmi vya umma vinavyotekeleza jukumu la hifadhi ya
jamii ndani ya nchi yetu. Niwapongeze si tu kwa kutimiza Miaka sabini,
mkitekeleza jukumu, wajibu na dhamana mliyopewa na taifa katika hifadhi ya
jamii bali pia kwa kutekeleza wajibu huo vizuri na kupata mafanikio makubwa
ambayo tumekwisha ambiwa hapa.
Mheshimiwa
mwenyekiti na ndugu wadau,
Mfuko huu umetoka mbali kama
sote tulivyoshuhudia na pia umepitia changamoto mbalimbali lakini leo tunayaona
mafanikio makubwa. Kabla ya uhuru tumesikia kuwa Bodi ya Mfuko iliundwa na
machifu na baadhi ya wazungu. Nijambo la
kushukuru kwamba hata wazungu wale waliuona umuhimu wa kuwa na sekta rasimi ya
hifadhi ya jamii, ambayo iliwalenga wazawa wa taifa hili. Hii inabainisha
umuhimu wa sekta hii kwa nchi na dunia kwa ujumla. Hivyo, napenda kuwakumbusha
wenzetu wa LAPF na mifuko mingine, kwamba dhama mliyopewa na taifa ni kubwa
kwani imeshika tumaini la maisha ya baadaye ya kila mwanachama wa mfuko na pia
wategemezi wao. Kufanya kwenu vizuri katika sekta hii kunamchango mkubwa katika
kuboresha maisha na ustawi wa watu wa taifa hili na pia kukuza uchumi wa nchi
kwa ujumla.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka 15 iliyopita na hasa baada ya
Mfuko huu kuundiwa Bodi yake na kuufanya kuwa shirika la umma linalojitegemea,
tumeona mafanikio mengi sana nami nichukue nafasi hii kuwashukuru na
kuwapongeza sana Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi zilizosimamia mfuko huu kwa
vipindi tofauti. Lakini pia nawapongeza sana Menejimenti ya Mfuko huu kwa kasi
ya ukuaji na maboresho ambayo tunayaona. Nimtambue kipekee Mzee wetu Marehemu
Aloyce Bura ambaye aliongoza Mfuko huu tangu mwaka 1989 hadi 2007 alipostaafu.
Kwa kweli alijitoa sana kuhakikisha mfuko huu unaimarika siku hadi siku.
Namuombea Muungu aiweke roho yake mahali pema peponi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, maendeleo tuliyosikia leo yanatuonesha kuwa
tukidhamiria jambo litawezekana. Hii ni changamoto kwenu ninyi watendaji mlioko
hapa. Kila mmoja akiweka bidii na uadilifu katika nafasi anayoifanyia kazi
lazima tutaona mafanikio ambayo yatadhihirika kutokana na wananchi kuridhika na
huduma wanazopata toka kwenu na kuwavuta kwa wingi zaidi kujiunga na mfumo
rasmi. Lazima mjiandae kuipunguza sekta hisiyo rasmi kwa kuandikisha wanachama
wengi zaidi kutoka katika eneo hilo. Kuwepo kwa vikoba, SACCOS na taasisi za
aina hiyo, kunaashiria utayari wa wananchi kujiunga katika sekta ya hifadhi ya
jamii. Inawezekana uchache wa wanachama kutoka katika sekta hiyo kunatokana na
mifuko kuwa mbali na kuweka wigo kwa kujifunga katika sekta iliyorasmi au la
mifuko haitoi elimu ya kutosha kwa umma. Ni vyema sasa, mkaongeza kasi ya
kutafuta wanachama kutoka maeneo hayo ya ajira binafsi. Hii itaongeza wigo wa
hifadhi ya jamii kwa kuwafikia watu wengi zaidi badala ya kuendeleza fikra ya
kudhani mafanikio nikuwa na mafao mengi. Mnapofikiria kuwa na mafao mengi,
hivyo hivyo mfikirie namna mtakavyo wafikia watu wengi pia.
Niwakumbushe tu kuwa kwa
kweli Tanzania inaweza kufika mbali sana endapo sote kwa pamoja tukiamua kuleta
mabadiliko kila mmoja mahali alipo kwa kufanyakazi kwa ujuzi na umairi na hata
ubunifu pia.
Ndugu
Wadau
Hivi Majuzi nilizindua fursa
ya mikopo ya elimu kwa wanachama wa Mfuko huu. Kwa kweli hiki kilikuwa sio
kilio cha wanachama tu bali pia hata Serikali ambayo kwa muda wote imekuwa na nia
thabiti ya kuendeleza watumishi wake lakini kutokana na ufinyu wa bajeti
inashindwa kufanya hivyo.
Najua mikopo ya elimu watakayopewa
watumishi itawawezesha kuongeza ujuzi na hivyo wataongeza ufanisi wa kazi.
Lakini pia watumishi hao wataweza kupandishwa vyeo kutokana na ufanisi wao na
viwango vya elimu na matokeo yake watakuwa na mishahara mikubwa ambayo itakuja
kuwapatia pensheni nzuri huko mbeleni. Hivyo jambo hili walilolianzisha LAPF
kwa kweli ni zuri sana na la kuigwa na mifuko mingine.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Huduma kama hizi ndizo
zitakazowapatia imani zaidi wanachama kwenye Mfuko wao. Hata hivyo, nitoe rai
kwenu kwamba wanachama wenu wanao pia wategemezi ambao wanamahitaji makubwa
katika sekta hiyohiyo ya elimu ya juu. Angalieni kama inawezekana kutumia
dhamana yao ndani mfuko kupata fao la elimu juu kwa wategemezi wao. Wote
tunatambua ufinyu wa bajeti ya serikali katika mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga
na elimu ya juu. Hili ni soko zuri kwa mifuko kuongeza wanachama lakini pia
kutoa hifadhi ya jamii inayozingatia mahitaji halisi ya watu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Baada ya mifuko kutoa mafao
ni muhimu kwa waajiri kuhakikisha kuwa makato yanafanywa mara moja toka kwenye
mishahara ya watumishi waliokopeshwa na kuwasilisha fedha hizo katika mfuko,
kila mwezi bila kuchelewa. Tukumbuke kuwa wingi wa mafao ahundoi dhima ya mfuko
kutoa mafao ya kisheria. Hivyo fedha hizo zisiporejeshwa wanachama tutaathirika
na ni wazi mfuko utaondosha baadhi ya mafao ili uweze kumudu kutoa mafao ya
kisheria. Hilo halitakuwa jambo jema hata kidogo kwani zitakuwa ni jitihada
hasi za kuudhoofisha mfuko. Kamwe jambo hili halikubaliki na nilazima tulikatae
na kupambana na waajiri na wale wote ambao hawafikishi mafao ya wanachama
katika mfuko kwa wakati.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Nikupongeze wewe na bodi
yako, menejimenti na watumishi kwa ujumla kwa uzinduzi wa nembo mpya ambayo
tumeiona na kuelezwa maana yake. Inatia faraja kwa wanachama wa mfuko kutambua
kwamba nembo hii ni ishara kuwa LAPF
sasa itakwenda au kukua kwa kasi. Na kweli maendeleo tunayoona yanaonesha
ukuaji wa kasi wa Mfuko huu. Naomba muendelee na kasi hiyo kamwe kurudi nyuma
kwenu iwe mwiko.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Kama nilivyokwisha bainisha
hapo awali, bado tunachangamoto kubwa kuhakikisha
huduma hii inawafikia wananchi walio wengi zaidi. Kundi tunalolishghulikia
mifuko yote ni dogo sana ukilinganisha na wananchi wote wanaostahili kupata
fursa kama hii. Nawaasa mamlaka ya hifadhi ya jamii na mifuko yote kufanya
utafiti wa kina kuona namna nzuri zaidi ya kuwaandikisha na kuyajumuisha
makundi ya waliojiajiri kwenye hifadhi hii ya jamii. Kwa kufanya hivyo
mtaisaidia sana Serikali katika azma yake ya kuhakikisha kuwa makundi mengi ndani ya jamii wakiwemo wazee
wanapata hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa
Mwenyekiti
Najua kuna wakati katika
kutekeleza azma hii mtahitaji Serikali iingilie kati kwa kurekebisha au kutunga
Sheria zitakazoongeza wigo wa wachangiaji. Nitoe rai kwenu, kuandaa mapendekezo kupitia Wizara husika nasi
tutayafanyia kazi kwa haraka ili kufikia haraka malengo yaliyopo ya kisera.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, nimalize kwa kuwaomba waajiri na wadau mbalimbali
kufanya kazi bega kwa bega na Mfuko huu kwa kutekeleza majukumu yenu ili
hatimaye wanachama na wananchi kwa ujumla wanufaike na shughuli za mfuko huu.
Maeneo ninayoweza kusema ni pamoja na uwekezaji, elimu kwa wanachama hasa ya
maandalizi ya kustaafu, kuandikisha na kuwasilisha michango na maeneo mengine.
Nafikiri mkiweka ushirikiano wa karibu kila mmoja atanufaika na mashirikiano
mtakayofanya katika kutimiza azima ya taasisi yenu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Nimeambiwa
hapa kuwa kutokana na suala la ushindani kuna baadhi ya waajiri wanashirikiana
na mifuko kuhamisha michango ya wanachama na kuipeleka katika mifuko ambayo
hawajajiunga. Utaratibu huu sio mzuri na ni kinyume na Sheria, hivyo nawaasa
muache na msimamie vizuri uhuru huu ambao wanachama wamepewa badala ya kuleta
vuruga katika mifuko.
Mwisho kabisa nawapongeza
tena mfuko wetu wa LAPF kwa kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake na
kusherehekea siku hii katika mwonekano mpya kama tulivyoshuhudia kwenye nembo
yao. Baada ya kusema hayo naomba kusema sasa kuwa Mkutano wetu wa saba wa wadau
wa LAPF umefunguliwa rasmi.
Asanteni
kwa kunisikiliza.
Mhe. Waziri wa Nchi OWM - TAMISEMI
0 comments:
Post a Comment