Rais Jakaya Kikwete
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete
---
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni
mkusanyiko wa upuuzi mtupu madai kuwa yeye Rais alishiriki kumwokoa mtoto wake,
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ambaye
alikuwa amekamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa Urais ni taasisi kubwa sana nchini na hivyo yeye akiwa Rais hawezi
kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya
watu wanamsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.
“This is nonsense – ni mkusanyiko wa upuuzi.
Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna
hiyo,” amesema Rais Kikwete
usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014,
wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi katika Marekani kwenye Hoteli ya
Marriot Washington, mjini Washington D.C.
Rais Kikwete ambaye yuko
katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani alitoa majibu hayo baada ya
kuwa ameulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi, 2012 na Katibu
Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Wilbroad Slaa, madai hayo yamempeleka mahakamani.
Amesema Rais Kikwete: “Hatuwezi
sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na
ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na
mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika
kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.’
Amesisitiza Rais
Kikwete: “Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza
katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa
kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa.”
Kuhusu swali jingine
aliloulizwa kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na
uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa
Ridhiwani, Rais Kikwete amesema:
“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi
kufikiria hata kuiweka rehani. Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta
kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu
kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti,2014
CHANZO: BOFYA HAPA
0 comments:
Post a Comment