Rais Jakaya Kikwete
----
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameueleza mchakato wa
kutafuta Katiba mpya nchini na changamoto zake kama barabara ndefu yenye kona.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa mchakato huo, kimsingi, unatakiwa kuongozwa na ukweli kuwa Katiba
ni kuhusu wananchi wenyewe na maisha yao na wala siyo tu mchakato huo kuongozwa
na idadi ya Serikali – mbili ama tatu.
Rais pia amesema kuwa ni
dhahiri kuwa yapo mengi ambayo hayajakaa sawasawa katika mchakato mzima hasa
kuhusu jinsi Katiba mpya itakavyolinda maisha ya wananchi na kusaidia kuboresha
ustawi wao.
Rais Kikwete ameyasema hayo
usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014,
kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington wakati alipokutana,
akazungumza na kujadili na Watanzania
wanaoishi katika Marekani hasa kutoka maeneo ya jiji la Washington D.C., na
majimbo ya Virginia, Maryland, California na New York.
Akiwaeleza Watanzania
kuhusu hali ilivyo nchini – kisiasa na kichumi – Rais Kikwete amesema kuwa ni
kweli kuwa mchakato wa kutafuta Katiba mpya umekuwa unakabiliwa na changamoto
kadhaa katika siku za karibuni.
Rais Kikwete amewaambia
Watanzania hao: “Najua kuwa mchakato wa Katiba umekuwa na changamoto katika siku za
karibuni lakini kwangu mimi mchakato huo ni sawa na barabara ndefu ambayo
haikosi kona. Kona zitakuwepo lakini mimi ni mtu ambaye anaishi kwa matumaini
na ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendelea na hatimaye kufikia mwisho
vizuri kama tunavyotarajia wote.”
Rais Kikwete ameongeza:
“Aidha, naamini kuwa yapo mengi kuhusu Katiba ambayo hayajapata muda wa kutosha
wa kuyajadili katika Bunge la Katiba. Kimsingi, Katiba ni Katiba ya wananchi,
ni Katiba kuhusu maisha yao na ustawi wao. Hili jambo sijaona kama linaonekana
sana katika mjadala wa Katiba.”
Ameongeza:
“Mchakato wetu kwa muda mrefu umekuwa kuhusu idadi ya Serikali, ziwe mbili ama
ziwe tatu. Kwangu mimi, idadi ya Serikali ni muhimu, lakini naamini kuwa Katiba
iwe ni kuhusu maisha yenyewe ya wananchi na ustawi wao lakini mwelekeo mzima wa
Mchakato huo usiwe kuhusu idadi ya Serikali tu.”
Rais Kikwete amesema
kuwa anajua kuwa yamekuwepo maneno mengi kuhusu Katiba lakini akaongeza kuwa
anaamini majawabu ya changamoto na matatizo ya sasa ya mchakato huo
yatapatikana.
“Najua kuwa maneno yamekuwa mengi lakini siyo
ndiyo demokrasia ya wazi inavyofanya kazi lakini sisi katika Serikali hatuna
wasiwasi na hali hiyo. Ndiyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika nchi ambako
demokrasia inafanya kazi. Yale mambo yanayotusumbua kwa sasa yanazungumzwa na
vyama vyetu na naamini majawabu yatapatikana.”
Wakati huo huo, Rais
Kikwete amerudia kusema kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kisheria ambao
utalinda mapato yatakayotokana na mauzo ya rasilimali ya gesi nchini kwa kizazi
cha sasa cha Watanzania na vizazi vijavyo.
“Tutahakikisha kuwa tunaanzisha Mfuko Maalum
kulinda fedha zitakazotokana na mauzo ya gesi. Raslimali hii pamoja na fedha
ambazo zinatokana na rasilimali hiyo siyo mali ya kizazi chetu tu bali ni mali
ya vizazi vijavyo vya Watanzania”.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment