
Gazeti
la Kiingereza la The East African, Toleo Na. 1030 lililochapishwa
mwishoni mwa wiki, Jumamosi, Julai 26, 2014, limeandika habari yenye
kichwa cha habari “Ex-soldiers want $3m for covert Congo operation”,
ikiwa na maana kuwa wanajeshi wastaafu wanadai kulipwa dola za Marekani
milioni tatu kwa kushiriki operesheni ya siri katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Inadaiwa
katika habari hiyo kwa zaidi ya wanajeshi 400 wastaafu wa Tanzania,
wametishia kuishitaki mahakamani Serikali ya Tanzania, wakidai posho ya
zaidi ya dola za Marekani milioni tatu (sawa na karibu sh. Bilioni sita)
kwa kushiriki operesheni ya kivita ya siri katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo kati ya 2000 na 2003.
Inadaiwa
na gazeti hilo kuwa askari hao wastaafu walipelekwa Congo ili kutoa
mafunzo kwa Jeshi la Congo lakini baada ya kuwasili walisambazwa katika
maeneo ya Majimbo ya Katanga na Kivu Kusini kukabiliana na wapinzani wa
Serikali ya Rwanda wa Interahamwe na waasi wa Burundi – FDD.
Habari hiyo siyo ya kweli, kwa hakika ni upuuzi mtupu na inalenga kupotosha ukweli na kuwapotosha wananchi. Serikali inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao ili kuwawezesha wananchi kujua ukweli.
· Siyo
kweli kuwa Serikali ama Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilihusika kwa
namna yoyote kuwapeleka Congo Askari hao wastaafu kwa sababu kimsingi
walikwishakustaafu na hawakuwa tena Jeshini.
· Askari hao walijipeleka wenyewe Congo, kinyemela na kwa mipango yao wenyewe ambayo waliifanya na watu wanaowajua wenyewe.
· Hivyo, kama askari hao kweli hawakulipwa, kama inavyodaiwa katika gazeti hilo basi wao wenyewe wanamjua nani wa kumdai.
· Walichofanya
askari hao wastaafu ni kinyume cha sheria na Serikali ya Tanzania
iliitahadharisha Serikali ya DRC kuhusu suala hilo.
· Serikali
ya Tanzania isingependa kuhusishwa, kwa namna yoyote, katika suala hili
kwa sababu haikuhusika nalo hata kama washiriki walikuwa raia wa
Tanzania.
Serikali
inapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa hakuna askari wake halali
ambaye amepata kwenda Congo ama nchi nyingine yoyote kushiriki
opereshini ya kivita na mapigano kinyemela.
Askari
wote wa Tanzania walioshiriki ama wanaoshiriki operesheni mbalimbali
duniani wamefanya na wanafanya hivyo chini ya miavuli halali ya
kimataifa.
IMETOLEWA NA
MKURUGENZI IDARA YA HABARI (MAELEZO)
2/08/2014




0 comments:
Post a Comment