Mbunge
wa Ilala Mh. Mussa Zungu ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa Uzinduzi
wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam
(CBE) akikata utepe kuashiria uzindunzi wa maadhimisho ya chuo hicho
kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake katika hafla iliyofanyika leo
jijini Dar es salaam.
Viongozi
mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50
ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiangalia moja ya
picha ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
iliyopigwa wakati akifungua Chuo hicho Januari, 1965. Kutoka kushoto ni
Mkuu wa chuo hicho Prof. Emanuel Mjema, Mh. Musa Zungu (Mb) jimbo la
Ilala,Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda,Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo
hicho Prof. Mathew Luhanga na Prof.Eliuta Mwageni Makamu Mkuu wa Chuo
Utawala na Fedha.
Viongozi
mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50
ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiwa katika picha ya
pamoja wakiongozwa na Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu na Mke wa Waziri
Mkuu, Mama Tunu Pinda (katikati). Nyuma ni bango lenye picha ya
kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa
wakati akifungua Chuo hicho mwaka 1965.
Mke wa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda kwa
niaba ya wanafunzi waliosoma katika chuo cha Elimu ya Biashara Dar es
salaam akizungumza na wadau na wanajumuiya wa Chuo hicho wakati wa
uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo hicho jijini Dar es salaam.
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia)
akiwaongoza wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa
maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
Mke wa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda
(katikati) akizungumza akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo
cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Mathew Luhanga
(kushoto).Wengine Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema.
Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam wakiendelea na shughuli mbalimbali chuoni hapo.
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia)
akiwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa
maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
Wadau
mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo Cha Elimu ya Biashara wakifuatilia
matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka
50 ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
Kikundi
cha ngoma kutoka Jeshi la Polisi kikiongozwa na Afande Juma Boha Mnyaa
kikitoa burudani ya ngoma ya asili ya ya Kibati kutoka Kusini Pemba wa
uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)
jijini Dar es salaam.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Chuo
cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kimezindua rasmi maadhimisho
ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake huku wadau na wanafunzi waliohitimu
chuoni hapo katika fani mbalimbali wakipongeza hatua iliyofikiwa na chuo
hicho katika utoaji wa elimu bora nchini.
Akiwakaribisha
wadau mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo hicho waliohudhuria hafla ya
uzinduzi wa maadhimisho hayo leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo
hicho Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga
kuukumbuka na kuenzi mchango mkubwa alioutoa Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere katika kufanikisha kuanzishwa kwa chuo hicho.
Amesema
msingi wa kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 unatokana na kuwepo kwa
uhitaji mkubwa wa wataalam katika nyanja za biashara na sekta ya
uendeshaji viwanda uliokuwepo nchini
Ameeleza
kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wataalam wengi katika fani za
Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi ,
Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameweza
kuhitimu na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Kwa
upande wake mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mbunge
wa Ilala Mh. Mussa Zungu akizungumza akizindua maadhimisho hayo
ameeleza kuwa mchango wa chuo hicho unaendelea kuonekana kutokana na
baadhi ya wahitimu wa chuo hicho kushika nyadhifa za juu za kitaifa na
kimataifa.
Amesema
wataalam waliopitia katika chuo hicho wamekuwa chachu ya shughuli za
maendeleo serikalini, viwandani ,taasisi za elimu , afya na taasisi za
fedha.
“Ndugu
zangu ni ukweli usiopingika, chuo cha Elimu ya Biashara kimefanya mengi
yanayohusu utoaji wa elimu ya biashara kwa watanzania baadhi yao
wamekuwa maarufu na wameshika nyadhifa za juu ndani na nje ya nchi”
Mh.
Zungu ametoa wito kwa uongozi na wataalam wa chuo hicho kuimarisha
tafiti mbalimbali hasa katika eneo la sekta ya biashara kwa lengo la
kuendelea kutoa mchango kwa maendeleo ya jamii na taifa hasa katika eneo
la ujasiriamali, vipimo na mizani ,utumiaji bora na salama wa huduma za
kifedha za ki-elektroniki na uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho.
Aidha,
ameiomba serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa
kipaumbele katika kushughulikia ustawi wa Chuo hicho ikiwemo ujenzi wa
miundo mbinu, vyumba vya madarasa, maabara za kisasa na ofisi.
Naye
mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga
akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo amesema kuwa
maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho yataambatana na shughuli
mbalimbali kwa lengo la kukitangaza chuo hicho pia kukusanya fedha kwa
ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya chuo.
Amezitaja
shughuli hizo kuwa ni pamoja na uandaaji wa chakula cha hisani, kuandaa
machapisho, kutoa mafunzo ya muda mfupi ya elimu ya biashara kwa watu
mbalimbali wakiwemo wajasiriamali na uuzaji wa vitu mbalimbali.
Aidha,
ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 mafanikio
mbalimbali yamepatikana yakiwemo ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi
wanaodahiliwa kujiunga na masomo hadi kufikia kutoka 25 pindi chuo
kinaanzishwa hadi 14000 wa sasa, ongezeko la kampasi kutoka 1 hadi
kufikia 4.
Mafanikio
mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi
kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada ya uzamivu (PhD)
chuoni hapo pamoja na chuo hicho kuanzisha ushirikiano wa elimu na
vyuo vikuu vingine vilivyo nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern
Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia
TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.
Kwa
upande wake mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama
Tunu Pinda akizungumza kwa niaba ya wanafunzi waliosoma katika chuo
hicho amepongeza hatua ya chuo hicho kuadhimisha miaka 50 tangu
kuanzishwa kwake na kubainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake chuo hicho
kimetoa wataalam wengi.
“Ninapofika
chuoni hapa ninafarijika sana kwa sababu mafanikio yangu kielimu
yameanzia hapa nawaomba wanafunzi mnaoendelea na masomo muwe mabalozi
wazuri wa chuo hiki mkiwa hapa chuoni na baadaye mtakapokuwa mnatekeleza
majukumu yenu” Amesisitiza Mama Pinda.
Aidhaa,
ametoa wito kwa viongozi wa chuo hicho kusimamia rasilimali za chuo
hicho kwa kuwatumia wataalam wenye sifa wanaozalishwa chuoni hapo.
0 comments:
Post a Comment