Wakati jamii ikiwa bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi
na kusababisha kifo chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika
Kijiji cha Matongola, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya
kubainika mtoto wa miaka sita akiwa amefichwa uvunguni mwa kitanda na
kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama yake mzazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alikiri kutokea kwa
tukio hilo na kusema kuwa taarifa za mateso ya mtoto huyo zilifikishwa
Kituo cha Polisi wilayani Kilosa za saa za mchana jana, baada ya uongozi
wa kijiji na kata kutoa taarifa na tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa
ajili ya mahojiano zaidi.
Mama aliyefanya ukatili huo anafahamika kwa jina la Sala Mazengo ambaye
alimficha ndani mtoto wake aliyefahamika kwa jina la Devota Malole na
kumfanyia vitendo vya kikatili ikiwa pamoja na kutompa chakula, wala
kumfanyia usafi.
Baada ya kufichuliwa kutoka alipofichwa, mtoto huyo alionekana kuwa
dhaifu kiafya kutokana na kukosa lishe pamoja na mazingira aliyokuwa
akiishi kutoridhisha, jambo ambalo ni kosa kisheria, pia ukiukwaji wa
haki za watoto.
Inadaiwa kuwa tangu mwka 2009 Sala amekuwa akimficha mtoto wake huyo
ambaye sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya
kupatiwa vipimo na matibabu.
Hata hivyo, mwanamke huyo alipoulizwa alidai kuwa afya ya mtoto wake
ilikuwa mbaya tangu alipozaliwa kutokana na magonjwa ya mara kwa mara,
pia hali ngumu ya maisha ilichangia kudhoofisha afya ya mtoto huyo.
Alidai kuwa ana watoto sita, pia alikiri kumlaza chini mtoto huyo
kutokana na kuwa na kitanda kimoja, ambacho hakiwatoshi watoto hao.
Aliongeza kuwa hata chakula amekuwa akikipata kwa shida kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda Paulo alisema kuwa mwili wa mtoto huyo umedhoofu kutokana na
kufichwa ndani kwa muda mrefu na bado mwanamke huyo hajaeleza sababu za
kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
“Siwezi kutoa taarifa ya kidaktari, lakini kutokana na afya ya mtoto
yule na mazingira tuliyomkuta ni dhahiri alikuwa akipata mateso na
kufanyiwa vitendo vya ukatili. Hata hivyo, uchunguzi zaidi tunaufanya na
kwamba taratibu za kumfikisha mtuhumiwa huyo Kituo Kikuu cha Polisi
mkoani hapa zinaendelea,” alisema Kamanda Paulo.
Alisema kuwa mpaka sasa bado haijafahamika kama mtoto Davota ni mlemavu
au la na kwamba taarifa za afya ya mtoto huyo zitatolewa baada ya
madaktari kumfanyia uchunguzi wa kina.
0 comments:
Post a Comment