SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, July 17, 2014

MKATABA WA GESI WA STATOIL NA TANZANIA

Swali kwa TPDC: Kwanini Makubaliano ni tofauti na Mkataba Elekezi (Model PSA)?
Baada ya kuvuja kwa Mkataba wa kutafuta na kuzalisha Gesi Asilia (PSA) kati ya Serikali kupitia TPDC na Kampuni ya Norway ya StatOil na baada ya baadhi ya wachambuzi kuhoji kuhusu mkataba huo, Shirika la TPDC limetoa maelezo yake. Sio mara moja, sasa ni mara ya tatu. 

Kimsingi TPDC wanasema wachambuzi waliochambua nyongeza hiyo ya Mkataba hawana uelewa wa mambo haya na wanaleta siasa. Nadhani ni muhimu TPDC wakajikita katika kueleza kwa lugha ambayo wananchi wa kawaida wataelewa badala ya kusingizia uelewa wa watu katika masuala haya. Wizara ya Nishati na Madini haina uelewa wa pekee wa masuala ya Mafuta na Gesi kama wanavyotaka umma uamini. 

Kuna watanzania wengi tu wenye kufuatilia mambo haya na wenye uwezo mpana hasa katika masuala ya kodi katika tasnia hii. Ni wajibu wa TPDC kutoa maelezo yasiyo changanya wananchi na bora zaidi waweke mikataba hii ya Gesi na Mafuta wazi. Maelezo yaliyotolewa na TPDC mpaka sasa hayaeleweki na yana lengo la kuwachanganya wananchi kama sio kuwaongopea.
Swali la Msingi
Serikali kupitia “Model PSA” imeweka viwango vya mgawanyo wa mapato kati ya Mwekezaji na nchi. Viwango hivi ni vya mgawo wa mafuta au gesi asilia yanayozalishwa kwa siku. Mkataba huu elekezi upo kwenye tovuti ya Shirika la TPDC na ndio mwongozo wa majadiliano kwa mikataba yote. 

Kwa mujibu wa Mkataba huu elekezi uzalishaji wa gesi asilia unapokuwa wa chini kabisa (0 –249.999 MMscf kwa siku) mgawo kati ya Tanzania na Mwekezaji unakuwa ni nusu kwa nusu (50 – 50 ) baada ya mwekezaji kuondoa gharama zake zote za uzalishaji.
Iwapo uzalishaji umefikia hali ya juu kabisa ( 1500 MMscf na zaidi) mgawo wa Tanzania unakuwa asilimia 80 na Mwekezaji asilimia 20. Mwekezaji anaruhusiwa kuchukua mpaka asilimia 70 ya Gesi iliyozalishwa kufidia gharama za uzalishaji. Hivyo, kinachogawanywa ni asilimia 30 zinazobakia.

Mkataba uliovuja ( TPDC na StatOil hawajaukanusha) unaonyesha kuwa kiwango cha chini kabisa cha uzalishaji Serikali inapata asilimia 30 tu na Mwekezaji asilimia 70 licha ya kwamba tayari gharama zake keshajirudishia. Vile vile kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji mgawo unakuwa sawa kwa sawa! Swali la msingi hapa ni, Kwanini makubaliano na kampuni hii ya StatOil yanaenda tofauti na Mkataba elekezi? Je, mikataba yote 26 imekwenda harijojo namna hii? Maswali haya bado hayajajibiwa na TPDC.
Tuelewe
Mkataba wa Gesi Asilia au Mafuta ni makubaliano ya kugawana mapato yanayotokana na kiwango kilichozalishwa. Katika maelezo yao TPDC wanaeleza kuhusu kodi ya mapato, mrahaba na kodi ya huduma. Kodi ya Mapato na kodi ya huduma ni kodi ambazo kila mfanyabiashara nchini anapaswa kulipa. Ikumbukwe kuwa imechukua miaka 20 na kelele nyingi sana mpaka kampuni za Madini kuanza kulipa kodi ya mapato na ushuru wa huduma. 
Mpaka leo hii bado Halmashauri za Geita na Kahama zinahangaika na kampuni za Madini kulipwa ushuru huu. Kampuni za Madini na za Mafuta hutumia mikakati ya kupanga kukwepa kodi (tax planning measures) kwa kutumia Tax Havens na Mikataba ya Double Taxation Treaties. Hivyo TPDC kusema tutegemee kodi ya Mapato ni sawa na kuimba kama kasuku na baada ya miaka 20 tutajikuta kwenye lawama zile zile za sekta ya Madini. 

Kwenye baadhi ya mikataba, kodi wanayolipa wawekezaji hukatwa kwenye mgawo wa TPDC na hivyo kodi hiyo hulipwa na TPDC na sio Mwekezaji kama tunavyoaminishwa na Serikali.
Kuhusu mrahaba wa asilimia 5 napo kuna tatizo kwani kwenye mikataba ya Gesi Asilia Mrahaba unalipwa na TPDC maana ndio mwenye leseni na sio Mwekezaji ambaye ni kandarasi tu. 
Mikataba kadhaa imeandikwa kwa namna ambayo Mwekezaji akilipa mrahaba, anajirudishia kwenye mapato ya Gesi kama gharama. Hivyo kimsingi mapato yetu ya uhakika ni kwenye mgawo wa uzalishaji. Ndio maana tunapiga kelele kuhusu mkataba huu wa StatOil kwenda kinyume na Mkataba mwelekezi wa Serikali.
Tutaambulia kiduchu sana
Kwa kuchambua Mkataba huu kati ya Tanzania na StatOil ya Norway hesabu zinaonyesha kuwa Nchi yetu itapata mgawo kiduchu sana. Chukulia uniti 1000 za gesi asilimia zimezalishwa kwa siku. Uniti 700 zinachukuliwa na Mwekezaji kufidia gharama za kuzalisha gesi hiyo na Uniti 300 zinazobakia Mwekezaji anachukua uniti 150 kama mgawo wake wa faida (profit gas).

 Hivyo Tanzania itabakia na uniti 150 tu kama mgawo wake, sawa na 15% tu ya Gesi Asilia yote iliyozalishwa katika siku hiyo. Iwapo Mkataba elekezi ungefuatwa Tanzania ingebakia na uniti 240 sawa na 24% ya gesi asilia iliyozalishwa.
Natoa rai kwa vyombo vya habari nchini kuandika masuala haya bila kuyumba maana yanahusu utajiri wa nchi yetu. Dhahabu imebakia mashimo kwa sababu Tanzania ililala na watawala kuandika mikataba ya hovyo. Tusilale kwenye Gesi Asilia. Wakati wa kutaka mikataba kuwa wazi ni sasa. Huu mmoja tu wa StatOil tunaweza kupoteza shilingi 1.6 trilioni, hiyo mingine 26 je? Nchi itabakia kweli? Tusikubali majibu mepesi. Tutake mikataba iwekwe wazi. Uwazi huleta uwajibikaji.

Zitto Kabwe, Mb
17 Julai, 2014

0 comments:

Post a Comment