Oscar Pistorius akiwa amejaa majonzi ameanza kujitetea katika kesi ya mauaji inayomkabili kwa kuiomba radhi familia ya Reeva Steenkamp.
Kwa sauti ya kutetema, amesema alikuwa "akijaribu kumlinda" na amesema anashindwa kujua uchungu wanaoupata.
kesi, Afrika Kusini
Bwana Pistorius amesema anasumbuliwa na"ndoto za kutisha" na mara nyingi aliamka na kusikia harufu ya damu ya Bi Steenkamp.
Waendesha mashitaka wanasema Pistorius alimuua Steenkamp mwezi Februari 2013 baada ya kuzozana. Pistorius anasema alidhani ni jambazi.
Mwanaridha huyo mwenye ulemavu wa miguu amewaambia ndugu wa Bi Steenkamp kwamba "hakuna wakati ambao ameshindwa kufikiria juu yao tangu mkasa huu utokee".
"Naamka kila siku asubuhi na ninyi ni watu wa kwanza kuwafikiria, watu wa kwanza ninaowaombea. Sifahamu uchungu na mawazo na ukiwa ambao nimewasababishia ninyi na familia yenu.
" Nilikuwa najaribu kumlinda Reeva. Nawahakikishia kuwa alipokwenda kulala usiku ule alihisi kupendwa".
"nimejaribu kuandika maneno yangu mengi kwenye karatasi. Mara nyingi kuwaandikia. Lakini hakuna maneno yatakayotosheleza maelezo yangu."
Amesema anatumia dawa za kuzuia msongo wa akili na kukosa usingizi.
"Naogopa kulala, Nimekuwa na ndoto za kutisha, Nasikia harufu ya damu na kuamka nikiwa mwoga.," amesema.
Amesema kamwe hataki kumiliki silaha.