Na Anna Nkinda- Maelezo, Lindi
Wakazi
wa kata ya Msinjahili wilayani Lindi wametakiwa kutoogopa kuvuta umeme
majumbani mwao kwa kuhofu kuwa wakifanya hivyo wataonekana ni matajiri
kwani matumizi ya umeme ni ya gharama naafuu ukilinganisha na mafuta ya
taa.
Mwito
huo umetolea jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini wakati akiongea kwa nyakati
tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika
matawi ya Muungano, Jitegemee, Sinde na Mnali yaliyopo katika kata ya
Msinjahili wilaya ya Lindi mjini.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema ili
kuboresha maisha ya wananchi Serikali imejitahidi kupitisha umeme wa
gesi katika vijiji vilivyopo katika kata hiyo na kupunguza gharama ya
uvutaji ambazo ni nafuu jambo la muhimu ni kwa wananchi kuutumia.
“Kuwa
na umeme nyumbani kwako na kuutumia ni mwanzo wa maendeleo, hata watoto
wako wataweza kuutumia mwanga huo kwa kujisomea hasa nyakati za usiku
na hivyo kufanya vizuri katika mitihani yao”, alisema Mama Kikwete.
Aidha
Mjumbe huyo wa NEC pia aliwataka viongozi hao wa Halmashauri kuu ya
tawi kuwahimiza watu wanaowaongoza katika maeneo yao kutumia mvua
zinazoendelea kunyesha kulima chakula cha kutosha jambo ambalo
litawafanya kuwa na chakula cha ziada na hivyo kuepukana na kitendo cha
kuomba chakula kwa majirani.
Akizungumzia
kuhusu suala la uongozi Mama Kikwete aliwahimiza wanawake kutoogopa
kuomba na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo
ili waweze kupata nafasi ya kuongoza na hivyo kufika katika ngazi ya
maamuzi.
Mama
Kikwete alisisitiza , “Sisi wanawake tunakabiliwa na changamoto nyingi
na mtu pekee anayeweza kuziongelea changamoto zetu kiusahihi ni
mwanamke mwenyewe hivyo basi msiogope kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi wakati wa uchaguzi ukifika mkifanya hivyo kutakuwa na viongozi
wengi wanawake ambao wataweza kuwakilisha matatizo na mawazo yetu katika
ngazi za juu za uongozi wa chama na Serikali”.
MNEC
huyo alimalizia kwa kuwahimiza viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi
ya CCM kuishi maisha ya upendo, mshikamano na amani kwani jamii ikiishi
maisha hayo itaweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa
kushirikiana.
Kwa
upande wake katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Lindi Haji Tajiri
aliwataka viongozi hao kuwa waaminifu katika ndoa zao na kuepuka tabia
ya kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja (michepuko) kwa kufanya hivyo
wataepukana na ugonjwa wa Ukimwi.
“Chama
Cha Mapinduzi kinahitaji kuwa na watu wenye afya njema ili waweze
kufanya vizuri kazi za chama nawaomba muwe waaminifu kwa wapenzi wenu
mkifanya hivyo mtaepekana na Ugonjwa wa Ukimwi”, alisema Tajiri.
Katibu
huyo wa Jumuia ya Wazazi mkoa pia aliwaomba kinamama kuiga mfano wa
Mama Salma Kikwete ambaye anafanya kazi kubwa ya kujitoa katika shughuli
mbalimbali za kijamii na kutetea haki zao, wasichana na watoto na
kuongeza kwamba anastahili pongezi kwani yeye ni mama na mlezi wa
taifa.
Mjumbe
huyo wa NEC taifa akiwa katika kata ya Msinjahili alifungua mashina ya
wakereketwa wa CCM Jumuia ya wazazi katika tawi namba tatu la Sinde
na namba mbili la Mnali.
Mama
Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini
alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya
kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na
viongozi.