SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, January 16, 2014

Kamanda Mkadam Azungumza na Waandishi wa Habari

Kamanda Mkadam akionesha bastola iliyotumia katika uhalifu wa kumpora fedha mfanyabiashara katika maeneo ya rahaleo Zanzibar ikiwa na risasi zake kamili, ilihisika katika tukio hilo.. 
Kamanda Mkadam akionesha moja ya Silaha aina ya SMG ambayo ilikuwa haina magazine waliokuwa wakiitumia watuhumiwa wa uhalifu katika maeneo ya rahaleo na kuitupa katika eneo la msikiti wa muembeshauri.wakati wakikimbia.
Kamanda Mkadam akiwaonesha waandishi moja ya silaha aina ya Gobole,waliofanikiwa Jeshi la Polisi kumkamata mtuhumiwa wakati akijiandaa kwenda kufanya uhalifu maeneo ya mtoni.  
Waandishi wa habari wakifuatilia taarifa inayotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamanda Mkadam Khamis Mkadam, kuhusiana na uhalifu uliofanyika mwanzo mwa wiki hii katika maeneo ya Rahaleo na kumpora fedha shilingi milioni kumi na moja katika tukio hilo na polisi kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao, kwa ushirikiano wa Wananchi wa kwahani. 
picha kwa hisani ya zanzinews 

*************
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi  Kamanda Mkadam Khamis. 
******
Habari za mchana ndugu wanahabari, tumewaita ili kutoa  taarifa kwa wananchi juu ya tukio ambalo limetokea ndani ya Mkoa wetu ambalo kwa kiasi kikubwa linataka ufafanuzi kutokana na jinsi linavyozungumzwa huko nje.

Siku ya tarehe 13/01/2014 majira saa 9:55 jioni hapo Rahaleo kwa Mchina Tambi palitokea tukio la unyangani wa kutumia silaha. Tukio hili lilitokea wakati  Bw:  SAID SEIF SALAMI 34, Riami wa RAHALEO ambaye ni MFANYA BIASHARA wa vyakula anayefanyia biashara yake Kibanda Maiti na anaishi mtaa  wa  RAHALEO alipofanyiwa unyanganyi huo.

Mfanya biashara huyu alifunga biashara yake majira ya saa 9:45 jioni ya siku hiyo ya tarehe 13/01/2014 na kuchukua pesa za mauzo ya kutwa jumla ya T.sh 11,500,000/= ambazo alizifunga katika bahasha /mfuko wa kaki na kuondoka nazo kuelekea nyumbani kwa kutumia gari yake no. Z. 128 EW NISSAN Rangi ya silver. Alipofika maeneo ya Raha Leo Kwa Mchina Tambi ndipo gari moja yenye no. Z.866 EX aina ya SCUDO ilipomzinga kwa mbele na ghafla aliona watu watatu wametokezea wakiwa na silaha mbili, moja ikiwa ni bastola na nyengine ni SMG. Watu hao walimlazimisha kwa
 usalama wake awape ule mfuko wenye pesa. Kwa kuhofia usalama wake alitoa pesa zote  jumla ya  T.SH 11,500,000/=

Majambazi hao baada ya kitendo hicho cha kuchukua hizo pesa walikimbilia kwenye gari yao. Kitendo hicho kilifanyika mbele ya watu ambao walianza kupiga kelele za mwizi!, mwizi!, mwizi!, kelele ambazo zilimfanya dereva wa gari ya majambazi kuondosha gari na kuwaacha wenzao watatu chini.

Wakati huo wananchi walipiga simu Polisi huku juhudi za ukamataji zikiendelea.

Polisi walifika eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa mmoja asiye na silaha akiwa tayari amekamatwa kwa msaada wa wananchi. Mtuhumiwa huyo anaitwaMAULID ALI @ KIPARA. Juhudi ziliendelea kufanywa kuwafuatilia majambazi wengine walioondoka  eneo la tukio na silaha. Miongoni mwao jambazi mmoja alifanikiwa kuitupa silaha aina ya SMG isiyo na magazine na shuka la kimasai ambalo alikuwa amevaa Jambazi huyo kujaribu kubadilisha utambulisho wake. Silaha na shuka hilo la kimasai vilitupwa hapo eneo la ndani ya msikiti wa Muembe Shauri. Jambazi huyu aliruka ukuta na kutokomea upande wa pili.

Mtuhumiwa wa tatu aliyekuwa na pistol alikabiliwa na Wananchi wa maeneo ya Kwa Ali Natoo kwa kushirikiana na Askari wetu wa vyombo mbalimbali wakiwemo Polisi, KMKM, JKU na Mafunzo na walifanikiwa kumkamata akiwa na hiyo Pistol aina GLOG 17 ikiwa na  no. PPG 617 ikiwa na risasi zake17 ambayo alikamatwa nayo Mtuhumiwa huyo aitwaye GANGIRA CHARLES MSHANDETE 34, MSUKUMA WA DSM  anayesadikiwa kuwa ni mtumishi wa PCCB DSM kutokana na maelezo yake lakini pia kitambulisho na silaha yake vinaonyesha kumilikiwa na Taasisi hiyo.
Baada ya mahojiano kuanza, mtuhumiwa wa kwanza alitowa ushirikiano wa namna ya kumpata mshirika wao ambaye aliendesha gari la Majambazi, hivyo Mtuhumiwa huyo dereva alikamatwa maneo ya Shangani nyuma ya African House nyakati za Magharibi. Mtuhumiwa huyo wa tatu anaitwa KHAMIS FAKI HAJI 40, MSHIRAZI WA MWERA. Baadaye Mtuhumiwa huyo alitoa ushirikiano wa kuitoa gari iliyofanyia tukio ambayo tayari alikuwa ameshaificha ndani ya eneo la viwanda vidogo vidogo. Gari hiyo ina no. Z 866 EX aina ya SUZUKI ambayo ndiyo iliyotumika katika ujambazi.

Baada ya kukamatwa dereva huyo, mtuhumiwa wa kwanza aliendelea kutoa ushirikiano kwa kumvuta mtuhumiwa aliyeitupa Bunduki ya SMG pale msikitini Muembe Shauri. Ilipendekezwa itumike gari ya mtuhumiwa wa tatu ili kumfanya yule anayevutwa asishituke. Wapelelezi na Mtuhumiwa wa kwanza walienda hadi eneo walilokubaliana kukutana. Walipofika pale na ishara ilitolewa ili afike, lakini  wakati unafunguliwa mlango wa gari alibaini kuwa waliokuwemo ni Askari na hivyo alitimka mbio. Juhudi zilifanyika na akakamatwa. Mtuhumiwa huyo wanne anajulikana kwa jina la RAJAB MOHAMED BAKAR 25, MSHIRAZI WA KOROGWE TANGA. Licha ya mtuhumiwa huyu kujitambulisha kwa jina hilo wenzake wanamtambua kwa jina la CHRISTOPHER MKAAZI WA KIGOMA – MUHA. Mtuhumiwa huyu alipopekuliwa alipatikana na silaha nyingine ya Pistol aina ya Browning yenye namba TZ CAR 93480. Hizi ni namba mpya za silaha ambazo kupitia data base ya CAR DSM tunaweza kujuwa mmiliki halali wa silaha hii na jinsi gani imetoka mikononi mwake pengine inawezekan na yeye akawa ni mshiriki wa kosa la ujambazi. Pia pistol hiyo ilikuwa na risasi moja.

Kwa ufupi katika tukio hili silaha zilizokamatwa ni tatu ikiwemo SMG moja na pistol mbili na risasi 18 jumla.
Kuhusu mali zilizoibiwa pesa taslim T.sh 3,900,000/= zimepatikana na kwamba mtuhumiwa wa pili ndiye aliyekamatwa nazo pamoja na simu ya mlalamikaji, kadi ya Benki na leseni ya udereva. Katika sakata la ukamataji Mtuhumiwa huyu aliutupa ule mfuko wa pesa na mtoto mmoja aliuchukua na kukimbia nao. Juhudi zilifanywa na akapatikana akiwa ameshawakabidhi kaka zake ambao walirejesha jumla ya T.sh 3,900,000/= huku mfuko uliokuwa umehifadhi ukiwa umechanwa hali ya kuwa awali walipokabidhiwa na huyo mtoto mfuko huo ulikuwa umefungwa vizuri. Mtu mmoja anashikiliwa kuwezesha upatikanaji wa mali zilizobakia. Kwa jumla walikamatwa watu saba na kuhojiwa katika tukio zima.

Sambamba na taarifa hiyo napenda pia kuwaonyesha bunduki aina ya Gobore tuliyoikamata tarehe 03/01/2014 saa 1:00 usiku huko Fuoni  Mkoa wa Kusini Unguja pamoja na watuhumiwa watatu ambao walikuwa wanajiandaa kufanya ujambazi kwa BAKHRESA Mtoni Unguja walikamatwa wakiwa na silaha hiyo ya Gobore yenye kutumia risasi  za Shortgun

Watuhumiwa hao ni:-

  1. ISMAIL HAJI SADI @ GREY, MSUKUMA WA AMANI KWA MABATA
  2. ALI MOHAMED ALI@ BAB ALLY, FUNDI ALI, WA FUONI
  3. OMAR ISSA MOHAMED, MSHIRAZI WA DSM
Watuhumiwa hawa leo tarehe 16/01/2014 tumawapeleka Mahakamani.

Naomba kutumia nafasi hii kwa mara nyengine tena kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote kwa ushirikiano wao katika mapambano na majambazi tuliofanikiwa kuwakamata tarehe 13/01/2014.

Tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi lao la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazoweza kusaidia kuwakamata wahusika wa matukio kama haya ambao  lengo lao ni kujipatia mali kwa njia ya mkato lakini pia kuleta hofu na taharuki kwa wananchi.

Nawashukuru, Asanteni sana.

0 comments:

Post a Comment